Uzuiaji wa tiba Loliondo sasa watikisa nchi
Baadhi ya wagonjwa wakiwa wamebebwa na ndugu zao kusogezwa karibu na dawa inayodaiwa kutibu magonjwa mbali mbali, huko Loliondo.
Hali hiyo inatokea wakati Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Walali, akisema amepokea maelekezo ya la serikali ya kusitisha huduma ya tiba inayotolewa na Mchungaji huyo.
Haya hivyo, amesema kuwa wagonjwa wote waliopo katika kijiji cha Samunge watatibiwa kwanza kabla ya kuondoka.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii juzi ilitangaza kuwa imemuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha kusimamisha tiba hiyo hadi hapo kamati iliyotumwa na wizara kwenda Loliondo kufanya uchunguzi itakapokamilisha kazi hiyo.
Aidha, Walali alisema watu kutoka maeneo mengine ni marufuku kwenda Samunge na kwamba vitawekwa vizuizi katika njia zote za kuingia katika kijiji hicho.
Walali aliwataka Watanzania kutii tangazo la serikali kwa sababu lina nia njema ya kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutokea katika eneo hilo.
“Tangazo hili halina nia ya kufuta huduma hiyo isipokuwa kuweka mazingira yatakayokuwa salama kwa watumiaji,” alisema jana alipozungumza na NIPASHE kwa njia ya simu.
Alivitaka vyombo vya habari kuacha kupotosha maelezo ya serikali na badala yake vijielekeze katika kuelekeza umma juu ya umuhimu wa tangazo la serikali ambalo limekuja baada ya kushuhudia hali ilivyo huko Samunge.
Alisema mambo yaliyosababisha kusitishwa kwa huduma hiyo ni ukosefu wa vyoo, maji na hali ya usalama kwa wananchi.
HATUA YA SERIKALI YAPINGWA
Serikali ikitoa maagizo hayo, umati wa watu umeendelea kumiminika kijini kwa Mchungaji Mwasapile kupata tiba yake inayodaiwa kutibu maginjwa sugu kama kansa, kisukari na ukimwi.
Wananchi hao wanafuata dawa hiyo ambayo ni kikombe kimoja ambacho hutolewa na mchungaji huyo peke yake.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wa mbalimbali wa mkoa wa Arusha wameomba serikali kutengua uamuzi wake wa kusitisha huduma ya tiba ya Mchungaji Mwasapile.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakihojiwa na waandishi wa habari jijini hapo jana, Miriamu Shayo, alisema huduma hiyo ni muhimu sana kwa Watanzania wote hivyo serikali iache iendelee kutolewa kwa watu wake.
“Mimi naomba serikali itengue uamuzi wake wa kusitisha huduma hiyo kutolewa kwa sababu inawasaidia kuwaondolea maradhi watu wengi wenye maradhi sugu,” alisema Shayo.
Naye Elibariki Msangi alisema rushwa isinyemelee katika upatikanaji wa huduma hiyo na kusababisha watu wenye imani na dawa inayotolewa na mchungaji huyo kukosekana.
Msangi alisema serikali isaidie kuboresha mazingira ya kijiji hicho ili watu waendelee kuponywa na dawa hiyo.
“Watu wasitumie nafasi ya utoaji wa huduma hiyo kuomba rushwa kwa kufanya hivyo kutasababisha ugumu wa upatikanaji wa dawa inayotolewa na mchungaji huyo,” alisema Msangi.
Mfanyabiashara wa madini jijini hapa, Martin Langoya, amepinga hatua ya serikali kusitisha huduma hiyo.
Alisema kamwe hawataacha kupeleka watu huko kupata tiba labda kama mchungaji huyo atauawa.
Langoya ana magari anayoyatumia kusafirisha abiria wanaokwenda kupata tiba Loliondo.
Mkazi mwingine wa jijini hapa, Lengiyeu Memumli, alisema amepeleka ndugu zake wawili, mmoja akiwa mgonjwa wa kisukari na mwingine mgonjwa wa saratani.
ASKOFU LAIZER: SERIKALI ISITHUBUTU KUSITISHA
Wakati huo huo, Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer, ameishauri serikali kutositisha huduma ya tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapile, kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta vurugu na kuharibu mahusiano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Askofu Laizer alieleza kushangazwa na hatua ya serikali ya kusitisha kwa muda huduma hizo bila kuwashirikisha wadau ambao ni wananchi na kanisa.
“Si sawa kusitisha huduma zenye element (viashiria) za kiroho na si sawa kuchukua
hatua hii bila kuwashirikisha wadau na wadau ni wananchi na sisi,” alisema.
Alisema iwapo huduma hiyo itasitishwa ‘moto’ unaweza kuwaka na kusababisha vurugu kubwa miongoni mwa jamii.
“Mchungaji amepata karama hii kutoka kwa Mungu, na ninampongeza kwa
kuwa hakuiweka chini ya pishi, anaitumia kwa faida wengine…wangekuwa
wengine angehitaji kupata mgawo mkubwa kutoka kwa watu anaowahudumia.
“Tunamshukuru mtu aliyepata maono hayo na mambo haya sio matangazo,
watu mbalimbali wametoa ushuhuda wa kupona kwao,” alisema.
Alisema sio dawa hii inayoponyesha bali ni ishara tu na kinachoponyesha ni imani na maombezi.
“Hili la Loliondo sio jambo la kisayansi unaloweza kulipima kwenye
Maabara, ni suala la kiimani na maombi, utapimaje,” alihoji.
Alisema mti unaotumika kutengenezea dawa hiyo sio wenye sumu, lakini
hata kama ungekuwa ni sumu, Mungu ameubariki na watu wanapona.
Askofu Laizer ameiomba serikali na watu wenye mapenzi mema kusaidia
huduma ya mchungaji huyo iweze kuendelea.
“Ushauri wangu kwa serikali tusaidie huduma hii hiendelee kwa kadiri Mungu anavyopenda na wote wanaokwenda kule wanasema ‘amina.’
Alisema sio sawa kusitisha huduma hii hivi hivi. “Sasa Mungu unataka awape nini zaidi kwa wema wake wote aliowatendea,” alisema.
Alisema viongozi wa kanisa hilo wamekwisha kumtembelea mchungaji huyo na kubaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa katika eneo hilo ambayo yanahitajika kuboreshwa.
“Mchungaji anahitaji kusaidiwa na kanisa limeanza kufanya hivyo, tumeenda kule kuweka mikakati na tumeona anaelemewa na idadi kubwa ya watu … tumeweka utaratibu wa watu kumsaidia, haiwezekani mtu akafanya kazi saa 24,” alisema.
Alisema timu ya wataalam wa ujenzi imekwenda Samunge kufanya tathmini ya ujenzi wa mabanda mawili ambayo yataweza kutumiwa na watu wapatao 600 hadi 700 kwa wakati mmoja.
Alitaja mapungufu mengine kuwa maji, vyoo, chakula na malazi.
Pamoja na kumsaidia kwa hali na mali, Askofu huyo ameomba pia wamsaidie kwa kumuombea mchungaji huyo kwani ‘neema ya Mungu imefunuliwa miongoni mwa watu.
Hata hivyo, alisema wapo baadhi ya watu wasiopenda huduma inayotolewa na mchungaji huyo mstaafu kutokana na wivu na wengine kwa kukosa biashara fulani.
“Wale walioathirika kwa sababu ya kiuchumi sina sababu nao, lakini wale
wenye wivu naawaambia kuwa wamwache Mungu aitwe Mungu kwani wakati
mwingine Mungu aliteua viumbe dhaifu kuonyesha maajabu yake,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya watu wanajaribu wamshika Mungu pua na kujaribu kumwongoza wanakotaka wao na akasisitiza kuwa wamwache Mungu aitwe Mungu.
No comments:
Post a Comment