PAC Zbr yataka sheria ya fedha irekebishwe |
MWENYEKITI wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) visiwani Zanzibar, Omar Ali Shehe, ameishauri serikali kupitia upya sheria ya fedha, ili iwe na meno makali katika kukabiliana na tatizo la matumizi mabaya ya fedha za umma.Shehe alitoa ushauri huo jana, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, kinachoendelea katika ukumbi wa baraza hilo, ulioko Chukwani,mjini Zanzibar. Shehe alisema sheria zilizopo ni dhaifu na hazisaidii kukomesha vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za umma na kwamba kuna haja kwa serikali kuangalia upya sheria ya fedha. Shehe ambaye alikuwa akiwasilisha mapendekezo ya kamati yake katika kikao hicho, alisema kamati hiyo imegundua dosari nyingi katika mfumo wa matumizi ya fedha za umma. Alisema hata hivyo watu wanaojihusisha na vitendo vya kuhujumu fedha za umma, hawachukuliwi hatua na kwamba hata pale wanapoopatikana na na hatia, wanatozwa faini. Shehe ambaye ni Mwakilishi wa ChakeChake kisiwani Pemba, alisema adhabu zinazotolewa sasa kwa watu wanaopatikana na makosa ya matumizi mabaya ya fedha, ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa makosa hayo yanayofanyika katika taasisi za umma. "Chini ya kifungu cha 38 cha sheria ya fedha za umma Namba 12 ya mwaka 2005, adhabu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kukiuka sheria hiyo ni faini ya Sh 500,000 au kifungo cha miaka miwili jela," alisema mwenyekiti huyo wa kamati.Alisititiza kuwa adhabu ya aina hiyo hairidhishi na ni kichekesho kwa mtendaji aliyejikusanyia mabilioni ya fedha za umma, kwa manufaa binafsi. "Sheria za fedha zipitiwe tena na ikiwezekana zitoe adhabu ya kila kifungu kinachohusika na isiwe kwa ujumla kama ilivyo sasa, ili adhabu inayotolewa ilingane na wakati na uhalisia wa kosa lenyewe," alisema Shehe. Alisema taasisi nyingi za serikali visiwani Zanzibar, haziwajibiki ipasavyo na kwamba baadhi zinafanya malipo bila vielelezo na zinapofanyiwa ukaguzi, watendaji wake wanatoa stakabadhi za udanganyifu. Alisema taasisi zilizofanyiwa ukaguzi na kushindwa kutoa vielelezo na stakabadhi kuhusu matumizi ya fedha za umma, ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Ofisi ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais na Wizara ya Kilimo na Maliasili. Nyingine ni Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Maji na Nishati (Pemba), Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Baraza la Manispaa ya Zanzibar, Tume ya kupambana na Ukimwi, Shirika la Utalii, Shirika la Bishara la Taifa (ZSTC) na Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi (ZIPA).Hali kadhalika, Hoteli ya Bwawani na Chuo Cha Taifa Zanzibar (SUZA). |
No comments:
Post a Comment