Membe: Hatumtambui Gbagbo na Datus Boniface |
SERIKALI ya Tanzania ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU) imetangaza rasmi kutomtambua rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo na kusema kuwa ikiwa kutatokea vita dhidi ya rais huyo basi vita hiyo itakuwa ni vita halali kwa manufaa ya kidemokrasia. Aidha, kwa upande mwingine imebariki hatua zozote zitakazo amriwa kumtoa kiongozi huyo anayeng’ang’ania madarakani licha ya matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Novemba kuonyesha ameshindwa. Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati akifafanua matokeo ya mkutano wa usuluhishi uliofanyika Mjini Addis Ababa, Ethiopia. “Tunajua uamuzi huu wa kutomtambua Gbagbo utaleta vita nchini humo, nitoe shaka kwamba ni bora iwe vita ya kutafuta demokrasia ya wananchi wa Ivory Coast…., itakuwa vita halali,” alisema Waziri Membe. Alisema katika kikao kilichofanyika mjini humo AU ilitangaza kumtambua mpinzani wa Gbagbo Alassane Quatarra kama Rais halali na si vinginevyo. Waziri Membe alisema jopo la viongozi watano; Rais wa Mauritania Mohammed Ould Abdel Aziz, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Idriss Deby wa Chad pamoja na Blaise Compaore wa Burkina Faso, kwa kauli moja walikubaliana kumtambua Quatarra. Kwa uchunguzi waliofanya wamegundua kwamba Quatarra, alishinda kwa asilimia 54 lakini baraza la Katiba likachakachua matokeo hayo. Katika kikao hicho Laurent Gbagbo alisusa kuhudhuria na badala yake alimtuma kiongozi wa chama chake Pascal Affi N'Guessan. Mwakilishi wake huyo alipinga uamuzi uliofikiwa ndani ya kikao hicho, na kwamba hawakubaliki kwa Gbagbo kuondoka madarakani. Wakati huohuo, serikali imetuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Japan kufuatia kutokea kwa maafa ya tetemeko la ardhi. Akitoa salama kwa niaba ya Rais Kikwete, Waziri Membe alisema Watanzania wako pamoja na taifa hilo katika kipindi hiki kigumu. Kwa upande mwingine Waziri Membe alielezea kuhusiana na taarifa ya kutekwa wa Watanzania 16 na waharamia nchini Madagascar, na kusema tayari Watanzania hao wameachiwa huru na mipango inaandaliwa ya kurudishwa nchini. Alisema maharamia hao wamekamatwa na wanatarajiwa kufunguliwa mashitaka kwa kuhusika na tukio hilo. |
No comments:
Post a Comment