Sunday, 13 March 2011

Loliondo yafurika tena

Waandishi Wetu, Loliondo na Dar

BAADA ya Serikali kubariki tiba ya magonjwa sugu yanayotolewa na Mchungaji Mstaafu, Ambilikile Mwasapile (76) katika kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro kimechochea umati mkubwa wa watu kufurika.

Mchungaji, Mwasapila jana alipongeza uamuzi wa Serikali kuondoa tishio la kuzuia kutoa dawa kwani watu wengi wamekuwa wakinufaika na dawa na mahitaji yanaendelea kuwa makubwa.“Tunamshukuru Waziri William Lukuvi kwa kuruhusu dawa iendelee kutolewa na kutoa ahadi ya kuleta huduma mbalimbali muhimu katika kijiji hiki,” alisema Mchungaji Mwasapile.

Ajali
Hata hivyo, huduma hiyo imekumbana na balaa baadaa ya baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa jana asubuhi.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mto wa Mbu kwa kuhusisha magari mawili ya safari za kitalii.Taarifa za polisi zilielezakuwa waliokufa katika ajali hiyo ni Raphael Kibonde (65) na mkewe ambaye jina lake kamili halikuweza kupatikana ambao walikuwa wanarejea kutoka Loliondo kunywa dawa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alimtaja mwingine aliyekufa katika ajali hiyo kuwa ni Beatus Morice (35). Maiti zipo katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.

Andengenye alisema idadi ya majeruhi haijafahamika kwa sababu walitibiwa katika zahanati ya Mto wa Mbu na kuruhusiwa na sita kati yao wamelazwa katika ya Mount Meru.

Chakula, malazi

Mmoja wa wasaidizi wa mchungaji huyo, Peter Dudui alisema jana kuwa kuanza kupatikana hudumu muhimu katika eneo hilo kama chakula, vyoo na mahala pa kulala kumechangia kupunguza wimbi la vifo vya wagonjwa.

“Sasa vifo hakuna, wagonjwa wanaokuja wanapata huduma kama chakula na maji na pia wanapata mahali pa kulala. Ingawa sehemu za kulala ni chache zinasaidia sana,” alisema Dudui.

Juzi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alitangaza kuwa Serikali imeruhusu Mchungaji Mwasapile kuendelea na huduma zake za tiba na kwamba itatoa ushirikiano wa kusimamia na kujenga mazingira mazuri ya kuendelea kutoa huduma.

Tamko hilo lilitolewa wakati ambapo tayari kulikuwepo na tetetsi kwamba Serikali imekusudia kumsimamisha Mchungaji huyo hadi hapo uchunguzi maalumu wa kitaalamu utakapofanywa kwa dawa yake.

Tangazo hilo la Serikali ambalo limetolewa wakati bado wataalamu wa afya wanachunguza dawa hiyo, limehamasisha maelfu kwa maelfu kumiminika kupata tiba.

Msururu mirefu ya magari yanayotoka Arusha mjini kuelekea katika kijiji hicho ambacho sasa kinaiitwa 'Kijiji cha Babu', jana ilionekana katika barabara ya Arusha hadi Ngorongoro.

Walioshuhudia msafara huo mrefu walisema kitu kibaya walichoshuhudia kwenye msafara huo ni madereva walombele kutoruhusu wenzao wanaookuja nyuma yao kwa kasi kutokana na kila mmoja kujaribu kuwahi kufika kabla ya mwingine kunywa dawa.

Baadhi ya watu walioshuhudia misafara hiyo, walisema ni vigumu madereva kuwaruhusu wenzao wanaokuja nyuma kwa hofu ya kuchelewa kwenye foleni ya dawa.

Vigogo wamiminika
Katika hatua nyingine vigogo wa serikali, wakiwemo, mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viogozi wa dini wanaendelea kumiminika kupata tiba ya magonjwa mbali sugu.

Miongoni mwao ni mawaziri wawili na wabunge kadhaa na wakurugenzi wa taasisi kubwa nchini.Viongozi wa dini walijitangaza wazi kutumia dawa hiyo na kupona magonjwa yao ni Askofu Thomas Laizer kutoka Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania  (KKKT) Dayosisi la Arusha, Askofu Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini na Paul Akyoo wa Dayosisi ya Meru.

Mwenyekiti SAU
Mmwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU) ameibuka na kudai amepona kisukari baada ya kunywa dawa ya Mchungaji Mwasapile.Kyara ambaye alienguliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alisema tangu anywe dawa hiyo inayotibu magonjwa sugu wiki moja iliyopita hivi sasa yuko ‘ fiti’ na kufafanua kuwa alikuwa na matatizo ya kisukari lakini kwa sasa afya yake imeimarika.

Alisema kutokana na watu mbalimbali wanaofuata tiba hiyo katika Kijiji cha Samunge, wakizuiwa kupata tiba hiyo hali ya usalama nchini itakuwa mbaya."Watu walishapoteza fedha zao kwenda kupata tiba, waliokwena nao wamepona sasa unafikiri wanakwenda watakubali kurudi nyumbani mwao bila kupea tiba," alisema Kyara.

Aliongeza: “Mimi nilikuwa Mwenyekiti wa tatu wa chama cha siasa kunywa ile dawa, watu ni wengi sana, hata hao waliotumwa kuchunguza kama dawa ina usalama nao baada ya kufika walianza kunywa. Watu wanaumwa sana, hapa Serikali itumia busara zaidi," alisema Kyara.

Huku akizungumza kwa furaha alisema, “Binafsi hali yangu kiafya imeimarika baada ya kunywa dawa ya mchungaji, wanavyosema kuwa watu wanakufa katika foleni si kweli, wanaokufa ni waliotolewa hospitali wakiwa mahututi," alisema Kyara.

Ujenzi mahema
Kampuni ya utalii ya Biq Expedition & Safaries, ambayo imekuwa ikileta watu katika kijiji hiki, pia imeanzisha mradi wa ujenzi wa mahema makubwa na kutoa huduma ya chakula katika kijiji cha Samunge.Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Nicholaus Minja alisema wameamua kuanzisha huduma hizo ili kushirikiana na Serikali kuhakikisha watu wanaofika kijijini hapo wanapata huduma muhimu.“Tumekuwa tukileta watu hapa, lakini tatizo limekuwa ni huduma nyingi hazipatikani tunaweka mahema na tutakuwa tunatoa huduma ya chakula ili kusaidia wagonjwa na ndugu,” alisema Minja.

Mgawo wa mapato

Wakati huo huo, imebainika kuwa mgao wa fedha za Sh500 ambayo ni gharama za tiba kutoka kwa mchungaji, Mwasapila imekuwa ikiwanufaisha watu wengine tofauti na matarajio kuwa anayenufaika ni mchungaji huyo.Mmoja wa wasaidizi wa mchungaji huyo, alisema katika kila Sh 500 anayopata, Sh 200 wanalipwa watu wanaokwenda kukusanya dawa porini, kuni na kuchemsha na Sh 200 ni sadaka ya Kanisa la KKKT Usharika wa Sonjo na mchungaji anayobakiwa nayo ni Sh100 tu.

Katika hatua nyingine, Tiba ya Mchungaji Mwasapile imepata umaarufu mkubwa jijini Arusha kutokana na kudaiwa kuwaponyesha wagonjwa wengi wa kisukari ambao baadhi walifikia hatua ya kuwa na matatizo unyumba.

“Babu kasaidia sana, watu wanarejea majumbani mapema, awali ulikuwa unakuta watu baa wakilewa tu hadi saa sita usiku, lakini sasa inaonekana amani imerejea nyumbani na wanaume wanarudi mapema,” alisema mmoja wa walionufaika na dawa huyo jina (linahifadhiwa).

Prof Lipumba
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema Serikali itegemee makubwa zaidi kuliko ya Loliondo.
Kauli hiyo ya Lipumba imetokana na umati wa watu kumiminika mkoani Arusha kufuata tiba zinayotolewa na mchungaji Mstaafu Mwasapile anayedaiwa kutibu magonjwa mbalimbali yanayomsumbua binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,  Profesa Lipumba alisema umati uliojaa kule Loliondo unaonyesha picha halisi kuwa Watanzania wengi ni wagonjwa, lakini sekta ya afya haina uwezo wa kuwahudumia kutokana na kukosa umakini.

No comments:

Post a Comment