Thursday, 17 March 2011

Jeshi la Polisi lajaribiwa

 
  Majambazi waua askari wawili kituoni
  Walikuwa wamewekwa mahabusu kituoni
  Waondoka na bunduki ya SMG na risasi
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha
Wimbi la uhalifu limetikisha Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kufuatia tukio la kuuawa kwa risasi kwa askari polisi wawili baada ya kuzidiwa na maarifa na majambazi waliokuwa wanashikiliwa kituoni.
Tukio hilo linaloamsha maswali mengi ya msingi juu ya usalama wa askari polisi, weledi wao kukabili wahalifu na hadhi ya vituo vya polisi nchini, pia limetoa changamoto juu ya mpangilio wa mambo katika vituo vya polisi kuhusu usalama wa askari na wote wanaofuata huduma kwenye vituo hivyo.
Tukio hilo baya la mauaji, limesababisha watuhumiwa 10 waliokuwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ujambazi na kuhifadhiwa katika kituo kidogo cha polisi cha Kagongwa wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, kukimbia.
Majambazi hayo wakiwemo raia wawili kutoka Burundi walikuwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ya mauaji ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Shinyanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lililotokea juzi majira ya saa 12:45 jioni.
Alisema watuhumiwa hao waliokuwa katika chumba cha mahabusu kituoni hapo waliwaua kwa risasi Konstebo F5344 Salimu na Konstebo F4964 Ngwengwe.
Kamugisha alisema siku ya tukio watuhumiwa hao wakiwa katika chumba cha mahabusu walimwita askari Konstebo Salum kwamba wanashinda naye na askari huyo aliitikia wito na kwenda.
Hata hivyo, alipokwenda alishtukia akipigwa kibao na mtu mmoja anayedaiwa kuwa alikuwa jamaa wa mahabusu hao kisha kumnyang'anya bunduki aina ya SMG namba 1430361 na kumpiga risasi.
Kamanda Kamugisha alisema Konstebo Ngwengwe aliposikia vurumani ndani ya chumba cha mahabusu alikwenda kutoa msaada, lakini naye ghafla alipigwa risasi sehemu ya kifuani na kufariki papo hapo.
Aliongeza kuwa mtu huyo alilivunja geti na mahabusu wote 10 waliokuwemo kutoroka.
Kaimu Kamanda huyo alisema baada ya mauaji hayo, majambazi hao walipora bastola aliyokuwa nayo Konstebo Salimu na kutoweka nayo.
Kamugisha alisema mahabusu hao walifanikiwa kutoroka eneo la tukio, lakini muda mfupi baada ya tukio, polisi kwa kushirikiana na wananchi wa mji mdogo wa Kagongwa na vijiji jirani, walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja, Audax Buberwa, na kumpa kipigo na kumsababishia mauti.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano na taarifa kuhusiana na watuhumiwa wengine tisa linaowasaka.
Aliwataja mahabusu waliotoroka kuwa ni Kwizela Lionel Ntahondilye Bartazar maarufu kwa jina la Hamisi (21), mfanyabishara wa Bujumbura na Lilakoz Willy maarufu kwa majina ya Nestory au Kalimanzila (29) ambaye ni dereva, wote kutoka Burundi.
Wengine ni Goodluck Leonard maarufu kwa majina ya James Leonard Kachenge au Bwashee au Papaa (26) ambaye ni dereva na mkazi wa Isamilo jijini Mwanza na Dar es Salaam na Selemani Dossi maarufu kwa jina la Tatii (33) ambaye ni dereva pikipiki mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Wengine ni Simon Fredy Sett (27), dereva wa pikipiki na mkazi wa Isamilo jijini Mwanza; Paul John Gulioma maarufu kama Babu (40), mkazi wa Nyasubi mjini Kahama na Kennedy William Lugazi (40), mkazi wa Nyamanoro jijini Mwanza.
Wengine ni John Peter maarufu kwa majina ya Ngosha au Hamisi, mfanyabishara ambaye ni mkazi wa Mwanza na Emmanuel Jackson (30) mchimbaji wa madini ambaye ni mkazi Mkuyuni jijini Mwanza na Runzewe wilayani Bukombe.

No comments:

Post a Comment