Tuesday, 22 February 2011

SADC Wataka Uchumi Uimarishwe Katika Bara la Afrika


Na Salma Said
JUMUIYA ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), imeeleza haja kwa nchi wanachama kuimarisha uchumi na kusifu amani na utulivu iliyopo hapa Zanzibar tokea kufanyika kwa uchaguzi mkuu Octoba mwaka jana.
Wakizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Mabalozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), waliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yao viongozi hao walitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa kuendesha uchaguzi uliokuwa huru na haki na ambao umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa.
Akitoa maelezo kwa niaba ya Mabalozi hao, Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Congo nchini Tanzania, Balozi Juma Alfani Mpango alitoa pongezi zake kwa watu wa Zanzibar kwa kuwezesha amani kubwa na inayoendelea hapa Zanzibar tokea kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Alisema kuwa hatua hiyo inaonesha wazi kuimarika kwa uongozi wa kisiasa hapa Zanzibar.
Aidha, viongozi hao walitoa salam zao za pole kwa Watanzania wote kutokana na tukio la hivi karibuni la miripuko ya mabomu lililotokea huko Gongolamboto mjini Dar-es-Salaam na kusababisha vifo, majeraha na hasara kubwa za mali za wananchi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Katika maelezo yake Balozi Mpango alieleza kuwa ushirikiano wa kisisa kati ka nchi za (SADC) bado uko mzuri na umepiga hatua kubwa.
Alisema kuwa hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na nchi wanachama wa (SADC) katika kuhakikisha uchumi wa nchi hizo unaimarika zaidi.
Alisema kuwa wawakilishi wa serikali za nchi za SADC wamekuwa wakiweka mikakati kwa kujitahidi kufanya kazi sana kwa ajili ya kukabili hali ya kiuchumi katika nchi zao.
Balozi huyo alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo nchi hizo zina wajibu wa kutumia fursa zilizopo katika nchi zao katika kuhakikisha hali ya uchumi inaimarika zaidi.
Walieleza kuwa Serikali ina wajibu wa kuendeleza kuimarisha miundombionu ya barabara na reli katika nchi wanachama.
Viongozi hao pia, walimueleza Dk. Shein kuwa SADC itatilia mkazo uimarishwaji wa sekta ya utalii ili iweze kuleta mafanikio zaidi.
Nae Balozi wa Zimbwabwe nchini Tanzania Mhe.Edzai Chimonyo alieleza kuwa nchi yake inaendelea vizuri katika kuhakikisha uchumi wake unaimarika zaidi ambapo hivi sasa umekuwa ukiimarika hatu kwa hatua.
Alisema kuwa hatua hizo pia, zimechangiwa na kazi kubwa inayofanywa na (SADC) na kusisitiza kuwa Jumuiya hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuondosha na kukabiliana na matatizo ya nchi wanachama, kazi ambayo imeweza kufanikishwa kwa asilimia kubwa.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa ujio wa Mabalozi hao wa SADC sanjari na pongezi walizozitoa kwa serikali na wananchi wa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi kwa salama.
Alieleza kuwa ujio wa viongozi hao ni dalili tosha kuwa kuna uhusiano na mashirikiano mazuri kati ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo na Zanzibar.
Dk. Shein alieleza kuwa SADC ina historia kubwa katika mapambano ya kimaendeleo ambayo yameanza tokea viongozi wakuu ambao walikuja na wazo la kuanzisha kwa Jumuiya hiyo ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi wanachama.
Alisema kuwa Tanzania imekuwa karibu sana na nchi hizo wanachama ambapo Zanzibar nayo imekuwa ikipata fursa mbali mbali za kielemu na nyenginezo kutoka katika Jumuiya hiyo.
Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa nchi wanachama kuja kuekeza Zanzibar katika maeneo mbali mbali hatua ambayo itaimarisha zaidi uhusiano katika nchi hizo.
Alisema kuwa katika sekta ya utalii Zanzibar ina sifa na vivutio vya pekee ambavyo niadimu kupatikana katika maeneo mengine ya nchi hizo, hivyo alitoa fursa kwa watalii kutoa nchni humo kuja kuitembelea Zanzibar.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza nchi za SADC kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha uchumi wake

No comments:

Post a Comment