Saturday, 26 February 2011

Pongezi polisi kwa kuanza kutambua haki za raia

                               
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema




Wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na
 Maendeleo (Chadema), jana walifanya maandamano ya amani  jijini Mwanza kupinga malipo ya fidia kwa kampuni ya Dowans, kuongezeka kwa gharama za maisha na kupanda kwa gharama za umeme. Maandamano hayo pia yalifuatiwa na mkutano  mkubwa wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho kikuu cha upinzani.
   
Maandamano hayo yaliyoridhiwa na Jeshi la Polisi, yalifanyika yapata miezi miwili tangu kutokea mauaji ya raia waliopigwa risasi na polisi jijini Arusha wakati walipokuwa wanajaribu kuzuia maandamano ya wanachama na wafuasi wa Chadema. Katika tukio hilo ambapo pia watu kadhaa walijeruhiwa vibaya, risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika katika jitihada za polisi kuzima maandamano hayo yaliyoandaliwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa meya katika jiji hilo.
   
Mauaji hayo na ukatiri mwingine uliofanywa na polisi dhidi ya wapita njia na watu waliokuwa wanaandamana kwa amani yaliamsha hasira na ghadhabu za wananchi wengi, huku wakimtaka mkuu wa jeshi hilo, Said Mwema ajiuzulu. Tangu wakati huo, uhusiano kati ya jeshi hilo na chama hicho umekuwa mbaya na malumbano yameibuka kuhusu upande upi hasa ulikuwa chanzo cha maafa hayo.
    
Hata hivyo, wananchi wengi walilinyooshea kidole Jeshi la Polisi kwa kusema kuwa halikuwa na sababu ya msingi ya kutumia nguvu dhidi ya watu waliokuwa wanaandamana kwa amani. Hoja ya Chadema ilitiwa nguvu na ukweli kwamba Jeshi la Polisi halina madaraka kisheria kuzuia au kuruhusu kufanyika kwa shughuli za kisiasa za vyama vya siasa, kwani sheria ya vyama hivyo ya mwaka 1992 inatamka bayana kuwa vyama hivyo vinatakiwa tu kutoa taarifa polisi ndani ya saa 48 ili vipatiwe ulinzi.
    
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa katika maandamano na mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika jijini Mwanza jana. Chadema kinasema kuwa kilitoa taarifa rasmi polisi Februari 20 kuhusu shughuli hizo za jana na ni jambo moja tu lililohitajika kufanyika ambalo ni makubaliano na jeshi hilo kuhusu barabara ambazo maandamano hayo yangepitia na uwanja ambao ungefanyika mkutano huo.
    
Hapa tunaweza kusema kuwa Jeshi la Polisi limeanza kutambua mipaka ya mamlaka yake kwa vyama vya siasa, hasa vyama hivyo vinapotaka kufanya kazi ya siasa. Kwa maneno mengine, jeshi hilo limetambua kuwa haki za raia ni pamoja na kukusanyika na kubadilishana mawazo kuhusu mambo yanayowafurahisha au kuwakera, ikiwa ni pamoja na kupinga au kuunga mkono sera au mipango ya serikali iliyo madarakani.
    
Matukio katika nchi za Libya, Misri, Tunisia na kwingineko katika Mashariki ya Kati yametufundisha kuwa haki haiombwi na jaribio lolote la watawala kuzuia maandamano ya kudai haki ni kukaribisha kusambaratika kwa tawala hizo. Tumejifunza kuwa katika hali hiyo, mshikamano wa watawala ghafla hutoweka,  kwani baadhi yao wasiotaka watu waonewe huongozwa na dhamiri zao na kujiunga na upande wa umma.
    
Tumejifunza pia kuwa ujio wa tekinolojia mpya ya habari kama simu za mkononi na mitandao mbalimbali imesaidia kuchochea mawasiliano ya watu katika muda mfupi, kwa maana kuwa sasa sio rahisi kwa watawala kuziba midomo ya watu hata kama watafunga magazeti, redio na televisheni. Ni kitanzi kwa watawala wasiopenda demokrasia na mabadiliko na wasiotaka kwenda na wakati.
    
Mikikimikiki inayozikumba nchi hizo hivi sasa imetufundisha kuwa, hakika huu ni wakati wa watawala kubadilika na kuwa watumishi wa kweli wa wananchi wao, kwani imedhihirika kuwa madikteta hawawezi kushinda nguvu ya umma.
    
Ndio maana tunalipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kufanikisha mkutano wa hadhara na maandamano ya wafuasi wa Chadema jijini Mwanza jana. Hiyo ni ishara tosha kuwa jeshi hilo sasa limeanza kutambua, kuheshimu na kulinda haki za raia.

No comments:

Post a Comment