Zitto: Sitambui kuvuliwa wadhifa wowote Chadema
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema)
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amesema hatambui kuvuliwa cheo chochote ndani ya chama hicho.
Alisema hadi sasa yeye bado ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kamati ya wabunge wa chama hicho iliyokutana mjini Bagamoyo Alhamisi iliyopita pamoja na mambo mengine kujipanga jinsi ya kutekeleza majukumu yao bungeni, iliazimia kumfukuza Zitto kwenye nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu kuvuliwa kwake nafasi hiyo na hatua ya wabunge wenzake kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
“Kuhusu mambo hayo waulize wabunge waliopiga kura hiyo watakujibu mimi bado ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, mimi bado naumwa niko kitandani jamani niacheni nipumzike,” alisema Zitto.
Akizungumzia kuhusu madai kuwa amelishwa sumu, Zitto alikanusha kupewa sumu na badala yake alisema anahisi kuwa alikula chakula kibaya.
“Sijapewa sumu, nimekula chakula kibaya na sijalishwa sumu na mtu yeyote kama watu wanavyosema,” alisisitiza Zitto huku akiomba aachwe apumzike.
Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya chama hicho, Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Zitto haitajazwa na mtu yeyote.
Lissu alisema kuwa kanuni za Bunge haziwalazimishi kuwa na mtu kwenye nafasi hiyo hivyo wameamua kuiacha wazi.
Juzi habari zilizovuja kutoka Kamati Kuu ya chama hicho zilidai kuwa kulikuwa na mkakati wa kuvua Zitto nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, baada wabunge wenzake kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Hata hivyo, jaribio hilo lilishindikana baada ya Kamati Kuu kukataa kura ya kutokuwa na imani na Zitto mpaka asikilizwe.
Habari zilisema kuwa wabunge walitaka kumtosa Zitto kutokana na kutofautiana na msimamo wa chama chake wa kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Novemva 17 mwaka huu. Kamati Kuu ya Chadema imeunda jopo la wazee wa chama chini ya Profesa Mwesiga Baregu kumsikiliza Zitto na matatizo yake na viongozi wengine wa chama ili kuleta suluhu ndani ya chama. Jopo hilo lina Shida Salum, Dk. Kitila Mkumbo (Katibu) na Nyangaki Shilungushela.
Akizungumza na NIPASHE juzi, Profera Baregu alithibitisha kuwa ni kweli amepewa jukumu hilo na Kamati Kuu kwa ajili ya kutafuta amani ndani ya chama hicho hasa kumsuluhisha Zitto na wabunge wenzake.
“Sijui ni lini lakini itakuwa hivi karibuni bado tunajipanga tukutane na Zitto tumsikilize matatizo yake na kazi yetu ni kujenga uhusiano mwema ndani ya chama, tunataka amani itawale ” alisema Profesa Baregu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment