Zanzibar Yahimiza Kero za Muungano kushughulikiwa
Na Zanzibar YetuSERIKALI ya umoja wa kitaifa Zanzibar imetaka suala la kero za Muungano kushughuulikiwa kwa dhati kwa kuzingatia sheria na taratibu wakati wa kutoa maamuzi pamoja na utekelezaji wake, kwa kuwa uzoefu unaonesha kumekuwepo na maamuzi yasio na utekelezaji wa jambo hilo.
Hayo yamebainika katika ya kikazi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu Hassan wakati akionana na viongozi wa wizara kadhaa wakati alipokwenda kujitambulisha hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema serikali zote mbili zinawajibu wa kuhakikisha zinasimamia kwa dhati shughuli za Muungano na zisizo za Muungano kwa faida ya Watanzania wote.
Aidha Dk Shein ametaka vikao vya pamoja baina ya pande mbili hizo za Muungano vinafanyika kwa kuzungumzia changamoto zilizopo na mana ya kukabilina nazo kabla ya kutolewa maamuzi ili kuondosha malalamiko ya muda mrefu yaliopo kati ya pande mbili hizo.
Alisema viongozi hao wanapokutana waamue mambo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu wakizingatia hoja za kimaendeleo kwa faida ya serikali zote mbili kwani kila upande una haki yake na mamlaka katika Muungano.
“Mimi nasema wazi mkiamua mambo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu itawasaidia sana katika utekelezaji wake, maana mkifanya hivyo yatakuwa yamebainishwa wazi katika Katiba ama ilani. Na pia ni vyema mkifanya kazi kwa kuaminiana na kushirikiana kwa karibu itaondosha ile khofu ya kuogopana na itasaidia kutatua kero zinazoukabili Muungano wetu” alisisitiza Dk Shein.
Katika ziara yake Waziri Samia alionana na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye kwa upande wake ametaka kuona mabadiliko katika suala la kero za Muungano.
“Tumezowea kufanya kazi kwa mazowea mara nyingi maamuzi yamekuwa yakifanyika kwa baadhi ya kero hizi za Muungano hutolewa maamuzi lakini ikifika wakati wa utekelezaji ndipo inapotokea tatizo na jambo kutopatiwa ufumbuzi wa uhakika ama kukamilishwa utaratibu wake kama lilivyoamuliwa katika vikao…sasa nadhani tufike pahala masuala haya yatekelezwe kama yanavyoamuliwa”. Alisisitiza Balozi Iddi.
Mbali na hayo amebainisha kuwa Zanzibar tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mambo yanaendelea vizuri kwa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao kama walivyokubaliana kwa mujibu wa Katiba iliyofanyiwa marekebisho na wajumbe wa baraza la wawakilishi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillah Jihadi Hassan ametaka kuwepo uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya pande mbili za Muungano ili wananchi wapate kujua kinachoamuliwa na kutekelezwa na serikali zao.
“Nashauri viongozi wenzangu tuache tabia ya kutatua matatizo kisiasa zaidi kuliko kitaalamu maana tumezowea kufanya hivi wakati mwengine tunaongeza tatizo badala ya kuyatatua panapokuwa na suala la ukweli basi huwa tunababaikababaika badala ya kueleza au kutekeleza suala hilo jambo ambalo halileti sura nzuri katika misingi ya utawala bora” alisema Waziri Hassan.
Waziri huyo mwenye dhamana ya habari nchini alisema tabia ya kuficha baadhi ya mambo kutasababisha wananchi kuwa na khofu na serikali yao na hatimae kutoa mwanya wa manung’uniko na minong’ono kitu ambacho hakitaleta sura nzuri kwa wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa maendeleo nchini.
Said Ali Mbarouk ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, yeye ameomba mashirikiano baina ya pande hizo mbili za Muungano yasiishie kuwa ya vikao tu pale inapobidi kukutana bali yawe ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo hususan kwa masuala ya miradi inayohusu pande mbili kwa kupeana taarifa kwa wakati ili kuweza kuimarisha ushiriki wa Zanzibar na utekelezaji wake.
Amesema kwamba wizara yake inatarajia kushirikiana kwa karibu sana na ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano pamoja na Wizara husika zinazohusiana na Wizara yake kutokana na changamoto kubwa zilizoko katika Wizara hiyo hususani suala la uvuvi katika bahari kuu.
Akitoa pongezi zake kwa kupokewa vizuri na viongozi hao, Waziri wa Muungano, Samia Hassan Suluhu amewashukuru viongozi wote alioonana nao kwa nyakati tofauti kwa kutoa maoni, mapendekezo pamoja na kueleza kwa uwazi changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano ili kuweza kusaidia kutafuta njia bora ya kuyapatia ufumbuzi ndani ya wizara yake inapoendelea na shughuli ya uratibu.
Waziri Samia, ambae alianza ziara yake siku nne ya utambulisho katika Ofisi na Wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, anatarajia kumalizia kesho kwa awamu hii kwa kukutana na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Vyombo vya Habari
No comments:
Post a Comment