Thursday, 23 December 2010

Waislam waandaa rasimu ya katiba mpya

Salim Said    

KILIO cha makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa katika kudai katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kimechukua sura mpya baada ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislaam (T), kuanza mchakato wa kuandaa rasimu ya katiba hiyo ambayo itawasilishwa serikalini ndani ya siku 30.
Hatua hiyo imekuja baada ya taasisi hiyo, kuamini kuwa suala la katiba mpya halina tena mjadala kutokana na umuhimu wake kwa taifa.

Hatua hiyo inakuja wakati taasisi  za kijamii, kisiasa, kidini na hata watu binafsi, zikiibuka na kudai  katiba mpya.
Siku kadhaa zilizopita Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema atamshauri Rais Jakaya Kikwete, kuangalia namna ya kuanzisha mjadala wa kitaifa, kama mchakato wa kuandika katiba mpya.

Lakinin kauli hiyo ya Pinda ilitofautiana na ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj  Ali Hassan Mwinyi, ambao kwa nyakati tofauti, walisema kwa sasa, hawaoni haja ya kuandikwa kwa katiba mpya.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislaam Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema kwa kuona umuhimu wa suala hilo katika mustakbali wa taifa, taasisi imeanza mchakato wa kuandaa rasimu ambayo wataiwasilisha serikalini.
“Kwa muktadha huu, tumeanza kuandaa mapendekezo muhimu ya Waislaam na Tanzania ya sasa na siyo ya jana katika katiba mpya, pia tutatahadharisha baadhi ya mambo katika katiba hiyo,” alisema Sheikh Ponda.

“Lengo ni kuhakikisha kwamba tunapata katiba inayokwenda na wakati, itakayojenga na kulinda haki, misingi ya usawa,amani na kuleta ustawi mzuri wa taifa.” alisisitiza.
Alisema rasimu hiyo itawasilishwa mara baada ya kukamilika na kwamba itajumuisha mawazo ya Waislaam wa mikoa yote nchini.

Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, mawazo hayo yatakusanywa kwa njia ya semina na makongamano maalumu kuhusu elimu juu ya umuhimu wa katiba mpya.

“Pia tunaomba kila Mtanzania mwenye mapendekezo mazuri ya kuivusha nchi yetu na kudumisha amani kwa ajili ya katiba mpya,  kuyafikisha katika ofisi za taasisi yetu au kwa kutumia anwani zake,” alisema Sheikh Ponda.

Alisema Waislaam wanaamini kuwa suala la katiba mpya ni la muhimu katika kuleta demokrasia na uhuru wa kweli.
"Suala hili si la mtu au taasisi moja kujifungia chumbani na kuandaa bali ni suala linalohitaji njia shirikishi kwa makundi yote ya kijamii," alisema.

No comments:

Post a Comment