Wednesday, 15 December 2010

Wageni wasio na vibali kutimuliwa


Imeandikwa na Flora Mwakasa

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji itaimarisha kazi ya kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini, wanakuwa na vibali halali na ambao vibali vyao vimekwisha, wanaondoka nchini.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha alipokutana na watendaji wakuu wa Idara ya Uhamiaji wakati wa ziara zake za kukagua shughuli zinazofanywa na idara zilizo chini ya Wizara hiyo.

Alisema, Wizara hiyo itafuatilia wakazi na wahamiaji haramu ambao wapo nchini kinyume cha sheria pamoja na wakimbizi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

“Katika nchi nyingine hasa za Ulaya, utakuta kama wewe ni mgeni na umefikia hotelini na kibali chako kimebakiza siku moja, basi unapewa taarifa na maofisa uhamiaji wanakutaarifu mapema kuwa umebakiza siku moja,” alisema Nahodha.

Alisema, Wizara yake itashirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kufuatilia wageni ambao waliomba vibali vya uwekezaji badala yake wanafanya biashara ndogondogo ambazo zinaweza kufanywa na wananchi wa kawaida. “

"Kumekuwa na malalamiko siku za hivi karibuni kuwa baadhi ya wageni walioingia nchini kwa vibali vya uwekezaji wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogondogo badala ya kuwekeza kama walivyoomba, suala hili linapaswa kushughulikiwa kikamilifu ili kuondokana na malalamiko ya wananchi,” alisema.

Nahodha aliwataka wananchi kushirikiana na Wizara kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwatambua watu hawa na wageni wengine wanaoishi nchini kinyume cha sheria ili wachukuliwe hatua.

No comments:

Post a Comment