Wednesday, 15 December 2010

Viongozi wasiotangaza mali kukiona





na Mwandishi wetu

KAMISHNA wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma, Jaji Mstaafu, Salome Kaganda, ameahidi kuwashughulikia viongozi wa umma ambao hawatatangaza na kuandikisha mali zao. Jaji Kaganda alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma.
Alisema katika kutekeleza sheria ya maadili ya viongozi wa umma, atahakikisha anawabana viongozi wote ambao hajatekeleza sheria hiyo kuitekeleza kwa kuwa ipo wazi.
“Nadhani sheria ya kuwataka viongozi wote kutangaza na kuandikisha mali zao iko wazi ... hivyo kwa kuwa nimepewa mamlaka hiyo, nitahakikisha nawabana wanaitekeleza,” alisema Jaji Kaganda.
Aidha Jaji Kaganda alisema atajitahidi; yeye haingii katika mkumbo wa makamishna waliopita katika nafasi ambao wanaelezwa kushindwa kuwabana viongozi wa umma ambao walikataa kutangaza na kuandikisha mali zao.
“Sitaki kusema kwamba wenzangu waliopita hawatekelezi majukumu yao, hapana!
wamefanya vizuri... lakini mimi kwa upande wangu nitahakikisha siingii katika mkumbo huo,” alisema Jaji Kaganda.
Jaji Kaganda ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kusini, Songea, hadi anastaafu, amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji mstaafu Stephen Ihema, ambaye amemaliza muda wake.
Uteuzi wa Jaji Kaganda ulianza Desemba 4 mwaka huu kabla ya kuapishwa jana.

No comments:

Post a Comment