Sunday, 19 December 2010

Uingereza kuendelea kuisaidia Zanzibar



UINGEREZA KUENDELEA KUISAIDIA ZANZIBAR

Na Ameir Khalid

Diane Corner - Our Ambassdaor

Balozi wa Uingereza Tanzania,
 Diane Louise Corner.


SERIKALI ya Uingereza imeahidi kushirikiana na Serikali ya Mapinguzi ya Zanzibar, katika kuendeleza maendeleo yaliyopo nchini ikiwemo kusaidia sekta ya afya ili wananchi waweze kuondokana na matatizo yanayowakabili.

Hayo yameelezwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diane Corner alipokuwa akifungua wodi ya wazazi ya hospitali ya Cottege Makunguchi Wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, Serikali ya Uingereza itaendeleza mafanikio zaidi kama yalivyofanywa katika kulifanyia matengenezo jengo hilo la wazazi ambalo litakuwa la kisasa na lenye vifaa vya kisasa.

Nae Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Duni Haji, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajali shida zinazowakabili wananchi wake katika kupata huduma ya afya pamoja na matatizo mengine yanayowakabili wafanyakazi wa sekta hiyo.

Alisema kutokana na matatizo hayo Serikali inaelewa na ipo katika hatua ya kuyafanyia kazi ili matatizo hayo yaweze kuondoka na kusema kuwa ni vyema kwa wananchi pamoja na wafanyakazi hao kuwa na subira kwani matatizo hayo hayawezi kuondoka mara moja.

Waziri huyo alifahamisha kuwa kampeni ya kuwahamasisha kinamama juu ya kufika hospitali wanapojihisi wakiwa wajawazito imefanikiwa kwa kiasi fulani na hivyo ufunguzi wa jengo hilo utawawezesha wananchi wa Wilaya ya Kusini kuweza kunufaika zaidi na huduma hiyo.

Aidha aliishukuru Jumuiya ya HIPZ kwa msaada huo wa ujenzi wa jengo hilo ambalo alisema litapunguza baadhi ya matatizo yaliyokuwa yanaikabili hospitali hiyo.

No comments:

Post a Comment