Saturday, 11 December 2010

Tanesco: Hakuna tena mgawo wa umeme

11th December 2010

Shirika la Umeme nchini (Tanesco)

Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limetangaza kumalizika kwa mgawo wa umeme nchi nzima kutokana na uzalishaji wa umeme kuongezeka maradufu katika vyanzo vyake vya uzalishaji nchini.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja Uhusiano wa Shirika hilo, Badra Masoud, alisema kuanzia sasa watanzania hawana sababu ya kuwa na shaka kuhusu kuwepo kwa umeme wa uhakika.
Alisema mitambo ya Songas nayo imeanza kuzalisha umeme hivyo kuongeza kiwango cha umeme kinachoingia kwenye gridi ya taifa.
Alisema hata mabwawa ya kuzalisha umeme yamefurika maji hivyo hakuna uwezekano wa kupungua kwa uzalishaji wa umeme.
“Watu wasiwe na hofu maana matatizo yaliyojitokeza yamekwisha kabisa, mvua zinanyesha kwa wingi sana na hakuna tatizo lolote kuhusu uzalishaji wa umeme,” alisema.
Alisema hata mitambo ya kufua umeme ya IPTL nayo imeanza kuzalisha umeme na kuingiza kwenye gridi ya taifa.
“Umeme unaozalishwa sasa unatosha kwa matumizi hivyo hakutakuwa na mgawo wa umeme kuanzia sasa,” alisema Badra .
IPTL juzi ilipewa mafuta na serikali na kuanza kuzalisha megawati 70 na kuingiza katika gridi ya taifa.
Mgawo wa umeme ambao ulidumu kwa siku kadhaa uliathiri shughuli nyingi za kiuchumi na kusababisha malalamiko kutoka kila kona pembe ya nchi.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila alikwenda mbali zaidi kwa kuelezea nia yake ya kuwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ang’oke.
Hata hivyo, Ngeleja alimjibu Kafulila kuwa kujiuzulu kwake hakuwezi kuwa suluhisho la matatizo ya umeme kwani serikali inaendelea kuyafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment