| Monday, 06 December 2010 08:44 |
WAKATI Mawaziri wawili kwenye baraza jipya, Samuel Sitta na Mathias Chikawe, wakiweka bayana nia yao ya kuendeleza vita dhidi ya ufisadi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam amesema hawataweza kutimiza azma yao bila kulilia kuandikwa kwa katiba mpya kwanza. Mhadhiri huyo wa siasa, Bashiru Ally, pia amewaambia makada hao wa CCM kuwa iwapo kilio cha katiba mpya hakitasikilizwa, basi wabadili mbinu kwa kulilia mjadala wa kitaifa na ikishindikana, wang'atuke. Sitta, ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Chikawe, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora- walieleza dhamira zao za kupambana na ufisadi huku wakisisitiza kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haina meno ya kuwashughulikia vigogo wanahojihusisha na rushwa na wanaotoa taarifa za uongozi kuhusu mali wanazomiliki. Sitta alisema baada ya kuapishwa kuwa atashinikiza kufutwa kwa sheria hiyo ili iundwe mpya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kupambana na ufisadi. Naye Waziri Chikawe juzi aliishukia Sekretalieti ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akidai kuwa imeshindwa kutumia mamlaka yake ya kuwaadhibu viongozi wanaokiuka maadili ya umma, akisema kuwa kila mwaka kuna kiwango cha bajeti ya serikali kinachoishia kwenye rushwa na ufisadi, lakini hakuna wanaoshughulikiwa. Lakini akizungumza jana na Mwananchi, mhadhiri Ally alisema kulingana na mfumo uliopo wa kisiasa, dhamira za mawaziri hao katika kupambana na mafisadi haiwezi kufanikiwa ipasavyo hadi hapo katiba mpya itakapopatikana. “Ili Sitta, Chikawe na mawaziri wengine waweze kutimiza dhamira zao za kupambana na ufisadi ni lazima washinikize uundwaji wa katiba mpya,’’ alisema Ally. Ally alisema kama mawaziri hao watashindwa kuliwasilisha hilo katika vikao vya Baraza la Mawaziri, waitishe mjadala wa kitaifa kama walivyofanya mawaziri wenzao nchini Kenya waliofanikisha juhudi za kuandikwa kwa katibampya. Kenya ilipitisha katiba mpya iliyotokana na utashi wa wananchi ambayo imepunguza madaraka ya rais, ukubwa wa Baraza la Bawaziri na kuzuia uteuzi wa mawaziri kufanywa kutoka kwa wabunge, lakini ikataba Bunge ndio liwathibitishe. Ally alifafanua kwamba kulingana na hali halisi ya mazingira pamoja na katiba ya sasa ambayo ni ya mwaka 1977, mfumo wa kisiasa unaohitajika nchini ni ule utakaowajibika moja kwa moja kwa umma na si kwa vyama. Mhadhiri huyo alikwenda mbali na kusema: “Kama wataona jitihada zao za kupambana na ufisadi wakiwa ndani ya serikali na CCM zinashindikana, wang’atuke na vijana wanaochipukia wafanye kazi hiyo.’’ Mara baada ya kuapishwa katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam, Sitta ambaye ni Spika wa Bunge la Tisa, bila hata ya kufafanua alikwenda mbali na kusema kuwa kama mambo ndani ya serikali yatakwenda ndivyo sivyo, ataangalia njia nyingine mbadala ya kutekeleza azma hiyo. “Ukiwa mpambanaji wa kweli, na uwaziri nilioupata ni fursa nzuri kwa mimi kupambana na ufisadi kwa kuwa nitakuwepo ndani ya serikali,’’ alisema Sitta. “Ili kuwabana vizuri mafisadi nitahakikisha sheria iliyopo ya maadili ya viongozi wa umma inafutwa na inaundwa upya.’’ Waziri Sitta alisema atatumia vikao vya Baraza la Mawaziri kuhakikisha maamuzi yoyote yanayofikiwa, yanafanywa kwa maslahi ya taifa na si kwa watu wachache na wajanja na kwamba kama juhudi zake hizo zitashindikana kutokana na mbinu chafu, ataangalia njia mbadala. “Ubutu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma iliyopo sasa ni miongoni mwa mambo yanayosababisha viongozi kuiba na kujilimbikizia mali. Dawa ni kufutwa na kutungwa mpya itakayoridhiwa na Watanzania wote,’’ alisema Sitta Chikawe ambaye katika Baraza la Mawaziri lililopita alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba, alisema pamoja na kudanganya, lakini pia wapo viongozi wa umma wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, lakini hakuna hatua zozote wanazochukuliwa na hivyo kupotosha dhana nzima ya utawala bora. Aliitaka sekretalieti hiyo kubadilika mara moja kiutendaji na kufanya uchunguzi wa kina juu ya maadili ya viongozi hao ili kuwafichua na kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaobainika kudanganya kuhusu mali walizonazo, kuhusika na rushwa au ufisadi. Kilio cha kutaka katiba mpya kimeibuka upya baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 ambao umeirudisha CCM madarakani na Chadema walionyesha kuwa wamepania kuongoza harakati hizo baada ya kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia. Chadema wanapinga matokeo ya uchaguzi wa rais na wanataka kuundwa kwa tume huru itakayochunguza mchakati mzima wa kutangaza matokeo hayo na pia wanataka kuundwa kwa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Kilio hicho kimeunganisha wadau kadhaa, ambao wameibuka na kusema suluhisho la matatizo mengi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ni kuunda katiba mpya itakayotokana na wananchi badala ya kuweka viraka kwenye katiba ya sasa. Hata hivyo, Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani alikaririwa akisema kuwa serikali haijapokea madai hayo ya katiba mpya na kwamba haiko tayari kwa suala hilo kwa kuwa uundaji katiba mpya hugharimu fedha nyingi. Waziri Kombani alisema msimamo wa serikali ni kuendelea kufanya marekebisho ya katiba na si kuiandika upya. |
Kheri yote inapatikana pale Mwenyezi Mungu anaporidhika na mja wake, na funguo za kheri zimo katika Dua pamoja na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuonesha kumpenda kwa kutenda yale yanayomridhisha na pia kumuogopa kwa kuepukana na makatazo yake. Mja anapokabidhiwa na Mola wake funguo hizi basi ajue kuwa Mola wake anamtakia kheri, na anaponyimwa basi ajue kuwa amefungiwa milango ya kheri
Monday, 6 December 2010
Sitta, Chikawe lilieni katiba mpya kwanza-Mhadhiri
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment