Monday, 20 December 2010

Dk Shein aahidi kuwasaidia wanawake






RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa anayoiongoza, itahakikisha inapambana na ubaguzi na madhila wanayofanyiwa wanawake.

Dk. Shein aliyasema hayo katika sherehe ya kumpongeza iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), iliyofanyika katika kiwanja cha Mwembekisonge mjini Unguja.

Akiuhutubia umati wa akinamama kutoka UWT mikoa mitano ya Zanzibar pamoja na wengine
kutoka Tanzania Bara, na wananchi waliohudhuria mkutano huo, Dk. Shein alisema atahakikisha wanawake wanapata huduma zote za muhimu pamoja na kushirikishwa katika maamuzi na shughuli za kimaendeleo.

Alieleza kuwa jambo moja kubwa ni kuhakikisha akinamama na watoto wanapata huduma nzuri za kiafya na kuhakikisha vijana wa kike wanapata elimu kuanzia ya msingi hadi chuo kikuu kwani uwezo huo wanao.

Alisema serikali anayoiongoza itahakikisha inapambana na vitendo vya udhalilishaji watoto na wanawake, vikiwamo vya kubakwa na mimba za utotoni.

Aliahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliomalizika kuwa, atapiga vita mila potofu zinazowakandamiza na kuwadhalilisha wanawake na watoto, jambo ambalo limesababisha kuunda wizara maalumu ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto ili isimamie ipasavyo masuala hayo.

Aliwahakikishia wanawake hao kwamba ombi lao la asilimia 50 katika nafasi za maamuzi atalifanyia kazi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT, Asha Bakari Makame, wakati akimkaribisha Dk. Shein alisema ushindi wa CCM unatokana na imani ya wananchi kwa chama hicho kutokana na kutekelezwa kwa vitendo Ilani na Sera za mwaka 2005 hadi 2010, ambapo Dk. Shein akiwa Makamu wa Rais akimsaidia Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.

Katibu Mkuu wa UWT, Amina Mwakilagi alisema sherehe kama hiyo tayari imeshafanyika Tanzania Bara ya kumpongeza Rais Kikwete kutokana na ushindi alioupata na ndio wakaamua pia, kufanya sherehe hiyo Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza Dk. Shein kwa ushindi alioupata wa urais wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment