Tuesday, 7 December 2010

Rais Shein, Maalim Seif wavalia njuga masuala ya afya





na Hassan Shaban, Zanzibar


RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ameanza kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayoikabili sekta ya afya baada ya kukutana na watendaji wakuu wa wizara hiyo katika kikao kilichohudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad. Akizungumza na watendaji wakuu wa wizara hiyo, Dk. Shein alisema serikali imedhamiria kuimarisha huduma za afya na kuipa hadhi Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa Hospitali ya Taifa ya Rufaa, itakayotoa huduma kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Katika kikao hicho, kilichofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Rais Shein, alisema serikali inatayarisha mpango wa kuzipandisha daraja baadhi ya hospitali vijijini ili ziweze kutoa huduma mbalimbali kwa malengo ya kuwaondolea usumbufu wananchi kufuata huduma mbali na maeneo wanayoishi.
Alisema hatua hizo ni utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, kama ilivyoelezwa katika ilani ya CCM, na kuwataka watendaji hao wakuu wa serikali kusimamia ipasavyo ilani hiyo.
“Serikali itazipandisha daraja baadhi ya hospitali za vijijini kuwa hospitali za mkoa kama tulivyoahidi katika ilani ya uchaguzi mwaka huu,” alisema Dk. Shein.
Kuhusu ugonjwa wa malaria, Rais Shein alisema Zanzibar ina uwezo wa kutokomeza kabisa malaria na kuwataka watendaji wakuu wa serikali kupanga mkakati madhubuti wa kudhibiti, licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa huo.
Katika kikao hicho, pia alihudhuria Waziri wa Afya na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Juma Duni Haji na Katibu Mkuu Kiongozi, Abdulhamid Yahaya Mzee

No comments:

Post a Comment