| |
| POLISI Kanda maalum ya Dar es Salaam, imeunda kikosi kazi maalum cha kiinterejensia (CRT) kwa ajili ya kupambana na uhalifu ikiwemo wale wanotumia nyaraka na mavazi ya jeshi hilo kuteka watu na magari. Kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es salaam, Suleiman Kova alisema wamepata taarifa kuwa kuna watu wanavaa mavazi ya jeshi hilo na kutaka kumteka nyara mwananchi mmoja akiwa na gari lake maeneo ya Kinondoni kwa Manyanya. Tanzania Daima Jumapili, ilipigiwa simu juu ya tukio hilo na mmoja wa watu aliyekumbana nalo ambapo alisema juzi majira ya jioni huko maeneo ya Kinondoni maeneo ya Ada Estate, alisimamishwa na mmoja wa askari feki kwa lengo la kumpa msaada wa kumpeleka Polisi Magomeni. Mwananchi huyo, hata hivyo baada ya kufika mbele maeneo ya Biafra, huyo alimshtukia askari huyo kufuatia sare yake hiyo kutokuwa na namba maalum za utambuzi, ndipo alipomtaka atoe kitambulisho. “Nahisi bila kuwa na uwezo wa kutambua hawa jamaa walikuwa na nia mbaya kwani walitaka kuniteka mimi na gari yangu,maana nilipomshtukia juu ya sare zake hizo, ndipo nilipomtaka anionyeshe kitambulisho na anitajie namba yake, lakini baada ya mweleza hivyo alianza kugoma,” alisema. Alisema aliamua kusimamisha gari maeneo ya Manyanya, ambapo hapo waliweza kutokea askari wengine ‘feki’ watano na kumhoji mwananchi huyo, huku wakisaidiwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wamelizunguka gari hilo. “Kwa ujasiri nao niliwatuliza na kuwataka kuonyesha vitambulisho vyao, lakini walinigomea, ndipo nilipobaini kuwa kumbe nao walikuwa na lengo moja kwani ni mtandao mpana wakisaidiana na watu mbalimbali,” alisema. Hata hivyo aliwatahadharisha wananchi hususan wanawake na wawe waangalifu pindi wanapotoa ama kuwapa misaada ya kuwapakia askari kwani wengi wanatumia mgongo huo kufanyia uhalifu kama ilivyo mtokea. “Askari feki wamezagaa kila kona, wananchi wanapaswa kuwa makini wawapo katika magari yao,wasikubali kupakiza askari bila kumwangalia kwa imakini, tunaomba jeshi la polisi kuliangalia hilo,” alimalizia Mwananchi huyo kwa kutoa tahadhari hiyo. Kamanda Kova, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alikiri kupokea taarifa za tukio hilo na kuchukua hatu za haraka ikiwemo kuimarisha ulinzi na msako maalum kwa kutumia kikosi kasi cha kiinterejensia cha CRT, ambacho alidai kuwa ni wataalum katika kubaini wahalifu wanaotumia nyaraka za jeshi hilo. “Mpaka sasa msako mkali unaendelea, taarifa za Mwananchi huyo zilitufikia muda mfupi, baada ya kukumbwa na hali hiyo, hivyo kikosi chetu maalum cha CRT, bado kinaendelea na msako mkali maeneo mbalimbali ilikubaini na kuwatia nguvuni,” alisema Kamanda Kova. Kamanda Kova alipongeza wananchi kwa kusherekea mkesha wa siku kuu ya Krismasi kwa amani bila matatizo kama inavyotokea miaka ya nyuma. ”Ulinzi umeimalishwa kila kona, wananchi wawetayari kutoa taarifa pindi watakaposikia ama kubaini vitendo vya kihalifu,” alimalizia Kova. |
No comments:
Post a Comment