na Hellen Ngoromera |
| CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kilichoko jijini Dar es Salaam, kinafanya utafiti mwingine wa chanjo ya virusi vya ukimwi (VVU) hapa nchini na Msumbiji. Hayo yalielezwa juzi jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Kisali Pallangyo, mbele ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa mahafali ya nne ya chuo hicho yaliyofanyika katika eneo la chuo hicho. Alisema utafiti huo unajulikana kama Programu ya Utafiti wa Chanjo Dhidi ya VVU nchini Tanzania na Msumbiji (TaMoVac) na unafanywa chini ya uongozi wa watafiti wa Chuo Kikuu Muhimbili na kwamba kwa sasa unaendelea kufanyika. Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo matokeo ya utafiti huo ni mazuri na yameleta msisimko kwa watafiti wa masuala ya chanjo dhidi ya VVU duniani pote. “…Hata hivyo napenda kusisitiza kwamba bado chanjo dhidi ya virusi vya ukimwi haijapatikana kwa hiyo ni lazima kila mtu awe makini katika kujikinga na maambukizi ya VVU,” alisema Profesa huyo. Akizungumzia kuhusu utafiti wa chanjo ya majaribio dhidi ya VVU jijini Dar es Salaam ulioanza mwaka 2007 Profesa Pallangyo alisema kazi ya utoaji wa chanjo hiyo umekamilika tangu Julai mwaka huu. Alisema kazi iliyopo kwa sasa ni kuona kama kinga hiyo itaweza kuua au kupunguza kuzaliana kwa VVU. “Kazi hiyo itafanyika kwa kuzihusisha maabara zetu. Aidha pamejengeka uwezo wa kitaalamu nchini wa kuendelea na tafiti za aina hii,’ alisema Profesa Pallangyo. Alirudia kusisitiza kuwa matokeo ya utafiti huo wa awali yameonyesha kuwa chanjo hiyo ni salama kwani hakukuwa na tukio lolote kubwa lililotokea miongoni mwa washiriki 60. “Chanjo hiyo imeweza kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU kwa asilimia 100 kwa washiriki waliopatiwa chanjo zote tano. Haya ni matokeo mazuri sana kupitia hata matarajio ya watafiti wetu pia ni ya muhimu katika harakati za kutafuta chanjo dhidi ya VVU. |
No comments:
Post a Comment