Friday, 24 December 2010

Krisimasi yapandisha gharama ya vyakula

na Janet Josiah

 

WAKATI Wakristo duniani wakiwa wanajiandaa kusherehekea sikukuu ya Krismasi kesho, bei za bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula, viungo na mavazi zimepanda kwa kiasi kikubwa.
Tanzania Daima lilifanya uchunguzi katika masoko mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kubaini kuwepo kwa gharama kubwa za bidhaa ambazo zimewashtua baadhi ya wanunuzi ambao wanajiandaa na sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Katika Soko Kuu la Kariakoo na Mwananyamala, uchunguzi wa bei za bidhaa umeonekana kupanda kwa kiasi kikubwa wiki hii tofauti na wiki iliyopita ambapo katika manunuzi ya viungo bei ya zamani ya tenga la nyanya liliuzwa sh 18,000 sasa sh 32,000 huku kilo ikiuzwa sh 1,000 sasa sh 1,500.
Gunia la karoti lilikuwa likiuzwa sh 35,000 sasa sh 40,000 huku kwa kilo awali iliuzwa sh1000 sasa sh 1,500 na Hoho gunia lilikuwa sh 50,000 sasa 60,000 kwa kilo ilikuwa sh.1,000 sasa sh 1,500.
Njegele awali gunia lilikuwa likiuzwa kwa sh 65,000 sasa sh 75,000 ambapo kilo awali iliuzwa sh 15,000 na sasa 2,000 na gunia la vitunguu swaumu lilikuwa likiuzwa sh 600,000 sasa sh 800,000 huku kilo ikiuzwa sh 6,000 sasa sh 8,000 hadi 10,000 katika baadhi ya maduka.
Bei hizo zimekuwa zikinunuliwa na wanunuzi wa hali ya kati huku wanunuzi wa hali ya chini ambao wamezoea kununua viungo vya mafungu wakipata wakati mgumu wa kufanya manunuzi kutokana bidhaa hizo kupanda bei.
Alipotafutwa Meneja wa Mipango na Biashara wa Soko Kuu la Kariakoo, Mrero Mgheni, kuzungumzia hali hiyo, alikiri vitu kupanda katika msimu huu wa sikukuu na kwamba endapo itakwisha hali itakuwa kama kawaida.

No comments:

Post a Comment