Sunday, 12 December 2010

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO

(PRESS RELEASE)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MKUTANO WA MAWAZIRI WANAOSHUGHULIKIA MASUALA YA WANAWAKE NA JINSIA WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU: UTAKAOFANYIKA KIBO PALACE , ARUSHA KUANZIA TAREHE 16- 18/12/2010

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Mashirika ya Kimataifa ya UNESCO, UNIFEM na UNFPA imeandaa Mkutano wa siku tatu (3) wa Kimataifa wa Mawaziri wanaoshughulikia Masuala ya Wanawake na Jinsia wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu utafanyika kuanzia tarehe 16 -18 Desemba, 2010 katika Jiji la Arusha, na unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 16 Desemba, 2010.


Nchi wanachama zinazotarajiwa kuhudhuria Mkutano huo ni kumi na moja (11) na wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo Brazzaville, Central Africa Republic, Sudan, Zambia, Angola na Congo DRC ambayo imependekezwa kuwa Kituo kikuu cha Kanda cha Utafiti na Uwekaji kumbukumbu masuala ya Wanawake miongoni mwa nchi wanachama.


Madhumuni ya mkutano huo ni :-
 Kuhuisha Sera na Programu mbalimbali zinazohusu masuala ya Wanawake na Jinsia katika nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu.

 Kusaidia, kuboresha na kueneza maarifa na kuongeza uelewa kuhusu maendeleo katika nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu kuwakaribisha watafiti na wataalamu mbalimbali.

 Kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na vyombo mbalimbali vya maamuzi.


Mkutano huo utakuwa wa tatu baada ya Mkutano wa pili uliofanyika Mombasa nchini Kenya mwezi Juni, 2009 ambao ulijadili mwendelezo wa pamoja wa utekelezaji wa Azimio la Kinshasa ambalo liliazimia kuanzisha Kituo cha Wanawake cha Utafiti na Uwekaji wa kumbukumbu katika Kanda ya Nchi za Maziwa Makuu. Kimsingi kila nchi mwananchama iliridhia jukumu la kuanzisha kituo chake cha kumbukumbu za masuala ya wanawake katika nyanja mbalimbali, na kituo kikuu miongoni mwa vituo hivyo kuanzishwa nchini Kongo DRC.


Mkutano huu pia utakuwa wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa Azimio la kuanzisha vituo vya taarifa na habari za wanawake. Uamuzi wa kuanzishwa kwa vituo hivi kwa ajili ya Utafiti na uwekaji wa kumbukumbu ulitokana na ukweli kwamba, bado nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na kijamii hali ambayo waathirika wakubwa wamekuwa ni wanawake na watoto.
Vilevile, imeonekana kuwa, mbali na kuwepo kwa matatizo hayo, nchi zilizopo Ukanda wa Maziwa Makuu zimendelea kukabiliwa na tatizo la ukatili kwa wanawake na watoto wa kike hali ambayo inasababisha athari ambazo zinaleta madhara miongoni mwa makundi hayo.


Aidha, kutokana na uwepo wa hali hiyo barani Afrika, nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ziliazimia kuweka msukumo wa pamoja katika kuhakikisha kuwa, haki na utu wa mwanamke kama ilivyoainishwa katika Azimio la 1325 la Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Usawa wa Jinsia unapewa msukumo wa kipekee.


Azimio hilo lilifikiwa katika Mkutano wa 32 wa Wanachama wa UNESCO October, 2010 ambapo UNESCO iliombwa kupanua wigo katika kushughulikia masuala ya wanawake na watoto waishio katika maeneo yaliyoathiriwa na vita au machafuko mengine. Baada ya makubaliano hayo, Idara ya masuala ya kijamii na haki za kibinadamu ya UNESCO, waliandaa mkutano wa kikanda uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia ili kuweka mikakati ya namna ya kulinda haki za wanawake katika maeneo yenye migogoro.


Miongoni mwa mambo yaliyoonekana katika kufanikisha azma hiyo ni uanzishwaji wa Kituo cha Wanawake cha Utafiti na Uwekaji wa Kumbukumbu za Wanawake na Jinsia miongoni mwa nchi wanachama wa Kanda ya Nchi za Maziwa Makuu.


Uanzishwaji wa vituo hivyo, unatarajiwa kuzinufaisha taasisi nyingine za Utafiti kupata taarifa mbalimbali kuhusu masuala ya Jinsia na Wanawake na kuziwesha kupata uzoefu wa namna ya kuboresha sehemu zao za taarifa ili kuwezesha uwepo wa vituo bora vya utafiti miongoni mwa nchi wanachama. Aidha, vituo hivi vitasaidia upatikanaji wa taarifa mbalimbali zinazozingatia jinsia.


Mkutano huo utakuwa chini ya uenyekiti wa nchi ya Tanzania na kusimamiwa na Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto.



Hussein A. Kattanga
KAIMU KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment