Friday, 17 December 2010

Jaji Mkuu akataliwa kesi ya samaki wa Magufuli


na Irene Mark
 South Korean fishing boat sinks in freezing Antarctic waters
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), imemtaka Jaji Mkuu Agustino Ramadhan kujitoa kwenye usikilizaji wa rufaa inayopinga masharti ya dhamana katika kesi ya uvuvi wa samaki kinyume cha sheria inayowakabili raia 36 wa kigeni.
Kusudio la kumkataa Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watatu wanaosikiliza rufaa hiyo liliwasilishwa mahakamani jana na Wakili wa Jamhuri, Stanslaus Boniface, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisilizwa.
Majaji wengine wanaosikiliza kesi hiyo ni Mbaruk Salim Mbaruk na Mohamed Chande Othman.
Hata hivyo, Jaji Mkuu alikataa kujitoa kwenye kesi hiyo na kuahidi kutoa uamuzi wake mwishoni mwa rufaa hiyo atakapotoa hukumu hivyo kuendelea kuisikiliza rufani hiyo kama kawaida ambapo alisema hukumu ya rufaa hiyo itatolewa kwa maandishi.
“Tumeamua kwamba tuendelee kusikiliza rufani hii na uamuzi utatolewa kwenye hukumu yote mwishoni,” alisema Jaji Mkuu kisha kuendelea kuwasikiliza mawakili wa utetezi wakiongozwa na John Mapinduzi.
Awali, wakili Boniface, alidai sababu za kumkataa Jaji Mkuu ni kauli zenye mwelekeo wa kuingilia kesi hiyo alizowahi kuzitoa kwa nyakati tofauti ambazo ziliandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Katika madai yake, wakili huyo wa Jamhuri alisema Jaji Mkuu aliingilia mwenendo wa shauri hilo nje ya Mahakama wakati akihutubia mkutano wa majaji wote nchini ambapo Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe (wakati huo), alikuwepo.
“Jaji Mkuu ametoa maelezo yanayohusu kesi hii sehemu mbalimbali alisema hayo katika hotuba yake kumkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria Mei 25 mwaka huu alisema hivyo… hata kwenye gazeti la Tanzania Daima la Juni 8 mwaka huu liliandika habari hiyo.
“…Mheshimiwa Jaji Mkuu alisema pia watuhumiwa wamenyimwa dhamana. Kwa sababu hiyo msimamo wetu ni jaji mkuu kujitoa kwenye shauri hili,” alidai wakili Boniface.
Kwa mujibu wa magazeti yaliyoandika habari hiyo, Jaji Mkuu alisema tatizo la kusuasua kwa uendeshaji wa kesi za jinai ambalo linahusisha mhimili wa Mahakama na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hayaleti picha nzuri katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Sehemu ya hotuba ya Jaji Mkuu inayolalamikiwa na ofisi ya DPP kwamba inaingilia mwenendo wa kesi hiyo ilieleza “Suala hili, lilipofunguliwa rasmi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 23, 2009 hadi lilivyohamishiwa Mahakama Kuu mwaka huu, muda umepotea bure kwa ukaidi.
“…Mwaka mzima washtakiwa wako rumande, wananyimwa dhamana mpaka mshtakiwa mmoja raia wa Kenya alifia gerezani hivi karibuni. Balozi wa China hapa nchini, alikuja kuniona juu ya wananchi wake kuwekwa ndani kipindi chote hiki, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba chombo chetu hakiioni hali hii.
“Hivi haitoshi kumshtaki nahodha wa meli, ambayo imekamatwa na kuwaachia hao watu wengine waende zao? Nimeongea na DPP Feleshi nikamuuliza kama hawezi kuwafutia mashtaka hao wengine… kubwa nililolipata ni kuwa anayemiliki meli hajulikani, lakini nahodha kashikwa tatizo liko wapi?” aliuliza Jaji Ramadhan.
Katika rufani hiyo, upande wa utetezi unapinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Jaji Njegafibili Mwaikugile wa Mahakama Kuu kwenye shauri namba 78/09 iliyotolewa Septemba 11, 2009 ambapo kila mshtakiwa alitakiwa kutoa kiasi cha sh bilioni moja.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba gharama ya samaki waliovuliwa kinyume cha kifungu namba 18 (1) cha Sheria ya Bahari kuu ya mwaka 2002 na marekebisho ya mwaka 2007 kwenye ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya Hindi ni sh bilioni 2.7 hivyo kwa mujibu wa sheria, watuhumiwa hao walitakiwa kulipa nusu ya gharama hizo.
Wakili Mapinduzi, alisema masharti ya rufaa ya jaji huyo yana makosa kisheria kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko kwenye hati ya mashtaka, mgawanyo wa kiasi cha dhamana kwa washtakiwa wote.
Alidai kwamba watuhumiwa wote kwa pamoja walitakiwa kulipa nusu ya gharama hizo badala ya kila mmoja kulipa sh bilioni moja, hata hivyo samaki waliokuwa kielelezo hawapo ambapo serikali imekubali kulipa kiasi cha sh bilioni 2.2 endapo itashindwa kesi hiyo.
Washtakiwa hao ni raia kutoka China, Vietnam, Indonesia, Filipino na Kenya walikamatwa wakiwa na samaki aina ya Jodari tani 296.32 na mazalia mengine ya samaki Machi 8, 2009 katika meli ya Tawaliq 1.


No comments:

Post a Comment