Saturday, 11 December 2010

Chami ataka TBS ifike Zanzibar



na Nasra Abdallah
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Masoko, Cyril Chami, ameahidi kupeleka mapendekezo ya sheria kwenye kamati maalum ya Bunge ili Shirika la Viwango Nchini (TBS) liweze kufanya shughuli zake hadi Zanzibar ikiwa ni katika kupunguza uingizaji bidhaa zisizokidhi ubora.
Chami aliyasema hayo jana wakati alipotembelea shirika hilo lililoko Ubungo Dar es Salaam katika kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo.
Chami alisema Muungano wetu ni muhimu hata katika kazi za TBS hivyo anajua wazi viongozi hawatashindwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo, kwani bidhaa feki zimekuwa si tu wa ajili ya kuathiri uchumi wa nchi bali hata afya za walaji.
Hata hivyo alilitaka shirika hilo kukaa pamoja na kuja na mapendekezo ambayo yataweza kumaliza uingizwaji wa bidhaa hafifu na feki na kuongeza kwamba suala hili linahitaji ushirikiano wa mamlaka zote na wizara zinazohusika kwa namna moja au nyingine.
“Ifike mahali tukubali kwamba suala la bidhaa feki ni tatizo la nchi yetu hivyo hatuna budi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo, katika hili tutaweza kukutana na wizara kama ya Mambo ya Ndani ambapo hawa watatusaidia kuona kwenye mipaka yetu kuna tatizo gani na njia za kuweza kukabiliana na tatizo hili,” alisema.
Aidha waziri huyo alitoa onyo kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakienda viwanda vya nchini China kuagiza bidhaa zilizo chini ya kiwango kwa nia ya kujipatia faida kuacha tabia hiyo mara moja kwani kiama chao kinakuja.
Kuhusu kutoa vyeti vya ubora kwa wazalishaji wa hapa nchini, Chami alilitaka shirika hilo kutoa upendeleo maalum kwa wajasiriamali wadogo kutokana na ukweli kwamba wao bado hawajakuwa na mtaji mkubwa ukilinganisha na wafanyabiashara wakubwa.
Alienda mbali zaidi na kuwaambia kwamba njia nyingine wanaweza kuwakopesha wajasiriamli hao au kuwalipisha fedha hizo kwa awamu kadiri watakavyozidi kuzalisha bidhaa zao na kuziuza lengo likiwa ni kuwasaidia nao waweze kukua.
Katika hili pia alipendekeza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kuwa na utaratibu wa kuwalipia wajasiriamali wao fedha kwa ajili ya kupata vyeti vya ubora kwa kutenga fedha katika bajeti yao.
Chami alilitaka shirika hilo pia kuweka kiwango kimoja cha bidhaa zinazoingia nchini na kutolea mfano kwamba siku hizi mtu unapokwenda dukani kuagiza dawa utakuta unaulizwa unataka ya Kenya, Italia au Tanzania ambapo yote haya alidai yametokana na ulegevu wa sheria zilizopo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika hilo, Charles Ekelege, alisema katika kukabiliana na uingizwaji wa bidhaa feki nchini, moja ya mamlaka wanazotakiwa kupata ushirikiano wao wa karibu ni Mamlaka ya Mapato (TRA) kutokana na umuhimu wake katika sekta ya uchumi.
Akitolea mfano alisema inashangaza sana katika kipindi cha mwaka 2010 na 2011 takwimu zao zinaonyesha kwamba ni shehena 22 za saruji zimeingia nchini, lakini kwa TRA takwimu hizo zinaonyesha kwamba ni 100, hivyo ukiangalia hapo ni shehena 78 hazikupimwa viwango vya ubora jambo ambalo ni hatari.
Ekelege alisema katika kukabiliana na matatizo hayo, shirika limekuwa likifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kufungua vituo kwenye mipaka ya nchi na kupima bidhaa katika nchi zinazotoka.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mpaka kufika Novemba mwaka huu jumla ya vyeti 11,312 vya kudhibiti ubora wa bidhaa kutoka nje vilitolewa.
Alizitaja changamoto ambazo wamekuwa wakizipata katika kutimiza wajibu wao kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa ubora.
Changamoto nyingine alisema ni uhaba wa fedha hasa katika kununulia vifaa vya maabara ambavyo vimekuwa vikiuzwa kwa bei kubwa.

No comments:

Post a Comment