JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
 Maswali mengi yanaulizwa kuhusu uraia, hasa wakati huu ambapo zoezi  la kuwabaini wageni wanaoishi nchini kinyume cha sheria linaendelea  katika maeneo mbalimbali nchini, yakitaka kujua nani hasa ni raia wa  Tanzania. 
Kimsingi, masuala ya uraia duniani kote yanaongozwa na falsafa kuu  mbili ambazo ni Haki za Kidamu (Jus Sanguinis - The rights of  blood), ambapo mtu hupata uraia kutokana  na uhusiano wa kidamu na wazazi wenye uraia wa nchi husika. Hii ina  maana kwamba, pamoja na mtu kuzaliwa katika nchi husika anatakiwa pia  kuwa na mzazi ambaye ni raia wa nchi hiyo. Falsafa hii ndiyo inayofuatwa  na nchi ya Tanzania. 
Kwa maana nyingine kuzaliwa pekee nchini Tanzania hakumpi mtu haki  ya moja kwa moja ya  kuwa raia wa Tanzania, bali mtu atakuwa raia  ikiwa amezaliwa Tanzania na wakati wa kuzaliwa kwake mzazi wake mmoja  sharti awe ni raia wa Tanzania.
Falsafa nyingine ni (Jus Soli - The right of Soil),  ambayo mtu  hupata Uraia kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi  ya nchi fulani. Kufuatana na Falsafa hii, mtu hupata uraia kutokana  na kuzaliwa katika nchi husika bila kujali uraia wa wazazi wake.
URAIA WA TANZANIA
 Masuala ya uraia nchini Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia ya  Tanzania ya mwaka 1995 Sura 357 kama ilivyorejewa mwaka 2002, pamoja  na kanuni zake za mwaka 1997. Sheria hii imeanisha aina tatu za uraia  wa Tanzania ambazo ni;
 1. Uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa 
 2. Uraia wa Tanzania kwa  kurithi
 3. Uraia wa Tanzania kwa Tajnisi, au kujiandikisha.
Uraia wa Tanzania wa  kuzaliwa:
 Utambuzi wa nani ni raia wa Tanzania unazingatia vipindi mbalimbali  vya historia ya Tanzania, yaani kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika,  kabla na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na baada ya Muungano wa Tanzania.  Pia, mahali alipozaliwa na alizaliwa na nani kama inavyoainishwa  hapa  chini:
 Aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru 
 Mtu aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru alitambulika  kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alizaliwa  Tanganyika na anatokana na Raia wa Uingereza, makoloni yake au nchi zilizokuwa  chini ya udhamini wa Uingereza
 Aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru 
 Mtu aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru alitambulika  kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja  wa wazazi wake alikuwa raia wa Tanganyika. 
 Aliyezaliwa Zanzibar kabla na Baada   ya Mapinduzi 
 Mtu aliyezaliwa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi alitambulika  kuwa ni raia wa Zanzibar wa kuzaliwa. 
 Ila, mtu huyo hakutambulika kuwa ni raia wa zanzibar ikiwa  wazazi  wake walitokana na mataifa yafuatayo; Australia,  Ubeligiji, Kanada, Ceylon (Sri Lanka), Ufaransa, Italia, New Zealand,  Ureno, Jamhuri ya Ireland, Afrika Kusini  na Marekani. 
Aliyezaliwa Tanzania siku na baada ya Muungano  wa Tanzania 
 Mtu aliyezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada  ya Muungano, atatambulika kuwa ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa ikiwa  mmoja wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.
Mtu hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kama wakati wa kuzaliwa  kwake hapa nchini, wazazi wake wote hawakuwa raia wa Tanzania; au Baba  yake ni Balozi wa nchi ya kigeni na ana kinga ya kibalozi; au mmoja  wa mzazi wake alikuwa ni adui wa nchi ya Tanzania (enemy) na mtoto huyo  alizaliwa katika eneo lililokuwa likikaliwa na adui.
 Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) ndiyo  sheria pekee inayotambua sheria zote za nyuma, zilizokuwa zinasimamia  masuala yote ya uraia katika vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania.
Kwa mantiki hiyo mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika  kwa kuzaliwa, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964,  ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa kuzaliwa,  mara baada Muungano. 
 Aidha, mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika  kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa ni raia wa Tanzania mara baada  ya muungano.
URAIA WA TANZANIA KWA  KURITHI:
 Raia wa Tanzania kwa kurithi ni mtu aliyezaliwa nje  ya Tanzania, na anatambuliwa kuwa raia wa Tanzania kutegemeana na kipindi  alichozaliwa na uraia wa wazazi wake wakati wa kuzaliwa kwake kama ifuatavyo:
 Aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla  ya Uhuru 
 Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya uhuru (akiwa ametokana na raia wa Uingereza  na Makoloni yake au himaya ya Mwingereza) alitambuliwa kuwa ni  raia wa Tanganyika kwa kurithi endapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
 Aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada  ya Uhuru na kabla ya Muungano
 Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano  alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi, ikiwa baba yake  alikuwa raia wa Tanganyika.
 Sheria ya Uraia ya Tanganyika ya mwaka 1961 haikutoa fursa kwa mama  kumrithisha uraia mtoto wake aliyezaliwa nje ya nchi. Hivyo mtu aliyezaliwa  nje ya Tanganyika katika vipindi tajwa hapo juu hakutambulika kuwa ni  raia wa Tanganyika kwa kurithi kupitia mama yake. 
Aidha, mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika hakutambuliwa kuwa  raia  wa Tanganyika kwa kurithi iwapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika  kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Raia wa kurithi hawezi kurithisha  tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanganyika.
 Aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla  ya Muungano wa Tanzania 
 Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano atakuwa raia wa  Zanzibar kwa kurithi endapo baba yake ni raia wa Zanzibar.
Vile vile, Sheria ya Uraia ya Zanzibar (The Zanzibar Nationality Decree,  CAP 39, 1952) haikuruhusu mama raia wa Zanzibar kurithisha uraia  kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar. Kwa maana nyingine, mtu  aliyezaliwa  nje ya Zanzibar katika kipindi hicho hakutambuliwa  kuwa ni raia wa Zanzibar kwa kurithi  kupitia kwa mama yake. 
Ieleweke pia kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar hakutambuliwa kuwa  raia wa Zanzibar kwa kurithi ikiwa Baba yake alikuwa  raia wa Zanzibar  kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Raia wa Zanzibar kwa kurithi  hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar.
 Aliyezaliwa nje ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania 
 Mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania siku na baada ya Muungano atakuwa  raia wa Tanzania kwa kurithi endapo mzazi wake mmoja ni raia wa Tanzania  kwa kuzaliwa au kuandikishwa/tajnisi.
Ni vyema ieleweke kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania hawezi kuwa  raia wa Tanzania kwa kurithi iwapo baba/mama yake ni raia wa Tanzania  kwa kurithi. 
Sheria ya Uraia Sura ya 357  ya mwaka 1995 (R.E, 2002) imetoa  fursa kwa mama ambaye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, tajnisi/kuandikishwa  kurithisha uraia wa Tanzania kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanzania.
Aidha, mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa  kurithi,  kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964  ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ile  ile mara baada Muungano. 
Mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika  kwa kurithi kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa raia wa Tanzania kwa  kurithi mara baada ya muungano.
Haya yameainishwa katika Sheria ya Uraia ya Tanzania Na.6, 1995 (Sura  357, Rejeo la 2002)  kifungu cha 30.
 URAIA WA TANZANIA KWA  TAJNISI (NATURALIZATION)
 Mtu yoyote ambae siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  kuzaliwa au kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa tajnisi kwa  mujibu wa Sheria ya Uraia Sura 357 ya mwaka 1995, (R.E,2002). 
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia  masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ndiye mwenye  mamlaka ya mwisho ya kumpa au kutompa uraia wa Tanzania Mgeni mwenye  sifa anayeomba uraia.
 Sifa za Kuomba Uraia wa Tajnisi;
 Mgeni anaetaka kuomba uraia wa Tanzania anapaswa  kuwa na sifa zifuatazo:
(i) Mwombaji awe na umri kuanzia miaka 18 na uwezo wa kufanya maamuzi  yanayokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi,
 (ii) Awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda  wa miezi 12 mfululizo kabda ya kutuma maombi ya Uraia, 
 (iii) Katika muda  wa miaka kumi  kabla ya miezi kumi na mbili hiyo  awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali kwa muda  usiopungua miaka saba. 
 (iv) Awe anafahamu vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza,
 (v) Awe na tabia njema,
 (vi) Awe na manufaa kwa taifa, yaani awe alichangia na anaendelea  kuchangia katika ukuzaji wa uchumi, sayansi na teknolojia na utamaduni  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
 (vii) Awe anakusudia kuishi moja kwa moja ndani ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa.
 Taratibu za kuomba uraia wa Tajnisi.
 Mgeni yeyote mwenye nia ya kuomba uraia wa tajnisi mwenye umri wa  miaka 18 na kuendelea anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo;
 (i) Mwombaji anatakiwa kujaza fomu za maombi ya uraia ambazo zinapatikana  katika ofisi zote za Uhamiaji za Wilaya, Mikoa, Afisi kuu ya Uhamiaji  Zanzibar na Makao Makuu ya Uhamiaji Dar es Salaam.
(ii) Mwombaji anatakiwa kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba Uraia  wa Tanzania mara mbili mfululizo kwenye magazeti yaliyosajiliwa Tanzania.
Mchakato wa Kushughulikia Maombi ya Uraia 
 Ili kuhakikisha kuwa wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa  kwa Taifa, maombi yote yanapaswa kupitia na kujadiliwa katika vikao  vya Kamati za Ulinzi na Usalama za:
Ngazi ya Kata au Shehia (kwa upande wa Zanzibar)
 Katika ngazi ya Kata au Shehia anayoishi mwombaji, ambapo atahojiwa  na maombi yake kujadiliwa na kikao hicho na hatimaye ombi lake kupelekwa  ofisi ya Uhamiaji Wilaya kwa hatua zaidi.
 Ngazi ya Wilaya
 Katika ngazi hii, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itajadili  maombi ya uraia yaliyowasilishwa kutoka ngazi ya Kata au Shehia, hatimaye  maoni na mapendekezo yake hupelekwa katika ngazi ya mkoa.
Ngazi ya Mkoa
 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nayo itajadili maombi yaliyowasilishwa  na kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na ombi husika na hatimaye  hutumwa kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ambaye atatoa ushauri na mapendekezo  yake kwa Mhe. Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia wa Tanzania  kwa maamuzi.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mwanamke aliyeolewa.
 Mwanamke mgeni ambaye ameolewa na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  wakati wowote wa uhai wa ndoa yake, anaweza kuwasilisha maombi ya uraia  wa Tanzania kwa tajnisi. 
Ombi la uraia kwa mwanamke aliyeolewa linatakiwa kuwasilishwa pamoja  na viambatanisho vifuatavyo;
(i)Cheti cha ndoa kilichosajiliwa na Mamlaka husika nchini 
 (ii) Pasipoti ya taifa lake ambayo haijaisha muda wake
 (iii) Kibali cha kuishi nchini ambacho hakijaisha muda wake (Hati  ya Mfuasi)
 (iv) Vielelezo vinavyothibitisha kuwa mume wake ni raia wa Tanzania.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mtoto
Sheria ya Uraia ya mwaka 1995  Sura 357 (RE 2002), inatoa fursa kwa  mzazi au mlezi halali wa mtoto (asiye raia) wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, kumuombea mtoto huyo Uraia wa Tanzania. Baada ya maombi rasmi  kuwasilishwa, Waziri mwenye dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto  huyo aweze kupata uraia wa tajnisi.
Waziri mwenye dhamana na masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo  ya Ndani) ndiye mwenye Mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa  Tanzania kwa mwombaji yoyote kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka  1995  Sura 357, rejeo la 2002.
 
 Makala hii imeandaliwa na
 Timu  ya Habari ya Operesheni Kimbunga -
 Oktoba, 2013