Saturday, 5 February 2011

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mlimani, FFU wapambana

 
  Mabomu ya machozi, risasi vyarindima
  Wanafunzi wawapiga Polisi mawe
  Tumaini, Usafirishaji bado tete
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakiwa katika maandamano ya kuishinikiza serikali iongeze fedha za posho ya chakula kutoka Sh. 5,000 wanazopewa sasa hadi Sh. 10,000.(Picha: Omar Fungo)

Wimbi la migomo na maandamano katika vyuo vya elimu ya juu limeendelea kutanda nchini jana, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kampasi ya Mlimani hali ikiwa ni mapambano baina ya Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) na wanafunzi waliokuwa wameanza maadamano chuoni hapo wakitaka kwenda Ikulu kuwasilisha kilio chao.
Hali ilikuwa ni ya kuviziana katika mpaka wa kampasi ya Mlimani na Chuo Kikuu cha Ardhi, ambako FFU waliweka ngome yao kuzuia wanafunzi waliokuwa wamenza maandamano kwenda Ikulu wasitoke nje ya mazingira ya chuo chao.
Kutokana na hali hiyo FFU waliamua kuwatangazia wanafunzi hao kutawanyika, lakini hawakutii amri hiyo, hivyo kulazimu matumizi ya mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na kuwatwanya wanafunzi hao ambao nao walijibu mapigo kwa kuwarushia mawe.
Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza, kwani wanafunzi hao waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, mengi yakielezea hali ngumu inayowakabilia kutokana na fedha kidogo ya chakula wanayopewa yaani Sh. 5,000 kwa siku, baadhi walikimbilia Chuo Cha Ardhi na kuwalazimisha wanafunzi wake waungane nao, lakini walikataa na kukimbilia madarasani.
Baada ya kuona wenzao wanawakimbia walianza kuwafurumusha kwa mawe ili waungane nao kuwakabili FFU. Wanafunzi hao walifurumusha mawe mengi ambayo yaliwalazimu FFU kujikinga vilivyo na ngao zao, huku wakisonga mbele.
Baadhi ya wanafunzi walikimbia hadi maeneo ya Makongo, ambako pia FFU waliwafuata huko.

No comments:

Post a Comment