TAMKO KUHUSU KATIBA MPYA
MUWAZA
waliotoa msukumo wa kuelekea kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania.
Wakati huo huo, inaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuukubali wito huo.
MUWAZA inaamini kwamba suala la katiba mpya limechelewa sana na inatoa
wito kwa serikali zote kulianzisha kwa haraka sana na kwamba lifanyike kwa
uwazi na ufanisi mkubwa. Aidha, Baraza la Wawakilishi (BLW) la Zanzibar
lichukue hatua za haraka kuwa mbele kwa maslahi ya Zanzibar katika
kupatikana kwa haraka katiba mpya ya Tanzania na hatimaye ya Zanzibar
kabla ya uchaguzi unaofuata.
MUWAZA inawapongeza wote waliotoa mawazo yao katika mustakbali wa
katiba mpya. Aidha, inampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa ya Zanzibar (SUK) kwa ujasiri na maelezo yake yanayotetea kupatikana
kwa katiba mpya.
MUWAZA inawaomba na kuwahimiza Wazanzibari wote kuungana na kuendelea
kutoa mawazo yao kwa nia ya kuipatia Zanzibar na Tanganyika serikali
zitakazoshirikiana katika muungano wenye haki sawa kwa washiriki wake.
Katika hatua ya sasa hivi, MUWAZA inapenda kutoa mapendekezo yafuatayo
kwa maslahi na mustakbali wa Zanzibar katika kuelekea kuipata katiba mpya
ya Tanzania:
1. Mchakato wa kuipata katiba mpya ya Tanzania uzingatie malalamiko,
kasoro (kero) na udhaifu wa muungano uliopo sasa ili katiba hiyo iweze
kuuimarisha muungano huo na kuufanya kuwa wenye uwazi, haki,
maslahi, kueleweka, kukubalika na kupendwa na washirika wake.
Mchakato huu uwe na uwakilishi wa serikali zote, wananchi, asasi za
kiraia, na wadau wengine na usiwe wenye kuendeshwa kwa utashi wa
chama fulani.
2. Katiba mpya ibadilishe mfumo mzima wa muungano na kuufanya kuwa
ni Shirikisho la Tanzania linalojumuisha Zanzibar na Tanganyika. Kwa
maana hiyo kuwepo na serikali tatu zenye marais wake kamili – yaani
Serikali za Zanzibar, Tanganyika, na Shirikisho la Tanzania.
‡ inawapongeza wanaharakati, wadau na wananchi kwa ujumla ‡
Wazanzibari wa ndani na nje ili kuleta utambulisho wa Wazanzibari na kuleta umoja
baina yao kwa kupigania mustakbali wa Zanzibar kama nchi, pamoja na kulinda
maslahi yake ya kidola, kitaifa na uhuru.
Mustakbal wa Zanzibar (MUWAZA) ni jumuiya iliyo ughaibuni inayowaunganisha Page 2 of 5
3. Katiba ya Shirikisho la Tanzania itoe heshima sawa kwa Zanzibar na
Tanganyika kama nchi kamili ili kulinda mamlaka na haki za nchi mbili
hizo. Maamuzi yote ya Shirikisho yapitishwe kwa makubaliano ya kura
za kila upande bila ya mchanganyiko. Mamlaka na utendaji wa Shirikisho
uwe na uwakilishi sawa kutoka kila upande wa Shirikisho.
4. SUK pamoja na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW) izingatie
jukumu zito iliyopewa na katiba ya Zanzibar la kuhakikisha kwamba
mipaka, mamlaka, rasilimali, heshima na utamaduni wa nchi ya Zanzibar
unalindwa kwa hali zote.
5. Katika kuyalinda mamlaka na haki za Zanzibar, BLW lipitishe kwa haraka
hoja/maazimio juu ya mambo mahsusi ambayo ni muhimu na lazima
kuwemo katika katiba mpya ya Tanzania. Pamoja na mengine, BLW
lizingatie kwa uchache mambo yafuatayo:
a. Zanzibar inaingia katika mchakato wa kupata katiba mpya ya
Tanzania ikiwa ni nchi kamili inayoshirikiana sawa kwa sawa na
Tanganyika katika mjadala huo. Kwa njia yeyote ile, Zanzibar
isiwe yenye kusukumwa katika majadiliano na maamuzi,
b. Serikali ya Zanzibar, rais wake, na bunge lake (BLW) ni sawa
sawa na serikali, marais, na mabunge ya nchi nyengine zilizo huru
duniani,
c. Rais wa Zanzibar pamoja na BLW wawe na mamlaka ya
kuyakataa maamuzi yeyote ya serikali ya Shirikisho la Tanzania
pale inapoona kwamba hayana mustakbali mwema kwa Zanzibar,
d. Kuyapitia upya makubaliano ya muungano na kujadili kila
kipengele na baadae kuyapatia makubaliano hayo mapya ya aina
ya Shirikisho ridhaa ya wananchi wa Zanzibar,
e. Kuhakikisha kwamba hata katika mambo ambayo yanabakia
katika mamlaka ya Shirikisho, Zanzibar inakuwa na kielelezo
chake kinachotambulika, (kwa mfano (a) maaskari/majeshi
waliopo Zanzibar wawe ni Wazanzibari na hawahamishwi kikazi
kwenda upande wa pili wa muungano au kinyume chake, (b)
mtiririko wa wageni wanaongia Zanzibar uwe unadhibitiwa kwa
njia na hati zinazokubalika, n.k.),
f. Shirikisho la Tanzania liwakilishwe katika Umoja wa Mataifa kwa
viti vya Zanzibar na Tanganyika. Kwa maana hiyo, Zanzibar
irejeshe kiti chake katika umoja huo na hivyo hivyo kwa
Tanganyika,
g. Zanzibar itambulike kama nchi kamili katika mikataba na
makubaliano yote ya kimataifa. Aidha, Rais wa Zanzibar awe ndie
mwenye mamlaka ya juu kwa Zanzibar ndani ya Shirikisho na
kimataifa,
Page 3 of 5
h. Mambo yote yanayohusu uhuru wa kiuchumi na kisiasa yabakie
ndani ya mamlaka ya Zanzibar. Aidha, mamlaka ya kuteua
wagombea uongozi na kuchagua yawe ni ya Wazanzibari
wenyewe. Kwa njia yeyote ile, masuala haya yasiingiliwe na
upande wa pili wa Shirikisho,
i. Urais wa Shirikisho uwe wa mtindo wa kupokezana baina ya
marais wa Zanzibar na Tanganyika katika kila muhula mmoja wa
uongozi. Kwa mfano, katika kipindi cha uongozi cha miaka 5,
miaka miwili na nusu iwe kwa Zanzibar na mengine miwili na nusu
iwe kwa Tanganyika,
j. Zanzibar ipate haki zake zote kutoka Benki Kuu ya Tanzania
(BOT) kulingana na mtaji wake wa uanzishwaji wa benki hiyo.
Aidha, Zanzibar iwe na kiwango cha ushiriki katika benki hiyo
kinachojuilikana kwa wastani wa asilimia kulingana na mtaji wake
wa uanzishi,
k. Mchakato na makubaliano ya katiba mpya ya Shirikisho la
Tanzania yafanyike kwa uwazi, haki, na ufanisi mkubwa na
kukamilika haraka iwezekanavyo kabla ya mwezi Juni 2012.
6. Katika kipindi chote cha mpito wa kuipata katiba mpya, ihakikishwe na
ionekane kwamba kanuni ya kupitisha sheria bungeni inayotaka thuluthi
mbili ya kura za wabunge wa Zanzibar inaheshimiwa ipasavyo. Vile vile,
mamlaka ya BLW kutoka ndani ya katiba ya Zanzibar juu ya kuidhinisha
au kukataa mabadiliko yanayohusu muungano inaheshimiwa.
7. Katiba mpya iwaelekeze marais wote kujiengua kutoka katika vyama
kabla ya kuapishwa ili wawe huru na misukumo ya vyama vyao na
wawajibike kwa mabunge yao. Kwa kufanya hivyo wawe na mrengo wa
ki-nchi badala ya ki-chama na waepukane na ukiritimba wa siasa za
chama kimoja.
8. Katiba mpya iondoe ulazima wa vyama kuwa vya kitaifa ili itoe uhuru wa
kuundwa vyama vya siasa vya aidha Zanzibar, Tanganyika, au Tanzania.
Sambamba na hilo, katiba mpya itoe uhuru wa kuwepo wagombea
binafsi wa kujitegemea.
9. BLW lihakikishe kwamba makubaliano ya mwisho ya katiba yanapitishwa
kwa kura huru za maoni kutoka kwa wananchi. Kura hizo mbili ziwaulize
Wazanzibari masuala ya (i) kuukubali muungano au kuukataa, na (ii)
kuikubali katiba mpya au kuikataa.
10.Mara baada ya mafanikio ya kupatikana kwa katiba mpya ya Shirikisho,
na kupatikana pia ridhaa ya Wazanzibari juu ya katiba ya Shirikisho
jipya, SUK kupitia BLW iipitie katiba ya Zanzibar na kuiandika upya ili
iendane na wakati. Kwa kufanya hivyo, SUK na BLW izingatie pamoja na
mengine mambo yafuatayo kwa nchi ya Zanzibar:
Page 4 of 5
a. Katiba ya Zanzibar iende sambamba na demokrasia ya vyama
vyingi na iwe yenye mwelekeo wa mabadiliko ya kuijenga
Zanzibar mpya yenye nguvu, maadili, utamaduni, amani na haki
sawa kwa wananchi wake,
b. Kutoa njia na fursa ya kusameheana na kusahau maonevu na
makovu yaliyopita katika historia kwa kuijenga Zanzibar mpya
yenye nguvu na upendo,
c. Kuzieleza, kuzitekeleza, kuzilinda na kuziheshimu haki za raia wa
Zanzibar bila ya kujali tofauti zao za ama itikadi, dini, rangi, asili
au jinsia,
d. Kutoa maelekezo ya kupata mahkama huru na tume huru ya
uchaguzi itakayowajibika katika mahkama iliyo huru,
e. Kuweka sheria imara ya uhuru wa vyombo vya habari pamoja na
uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari za ndani na nje kwa
wananchi wake,
f. Kuweka bayana haki ya Wazanzibari kushika nyadhifa za nchi yao
kulingana na ujuzi na uwezo wao bila ya upendeleo,
g. Kubainisha na kusimamia kisheria kwamba uongozi na utendaji ni
dhamana ya utumishi wa umma iambatanayo na uadilifu na
uwajibikaji, na kwamba dhamana hiyo sio haki miliki ya
mwananchi au kikundi fulani,
h. Kuzidisha mshajiisho wa kuyapa nguvu zaidi maridhiano na
kuboresha uendeshaji wa SUK pale panapostahiki,
i. Kuweka sera maalum za Zanzibar ambazo zitalindwa na kila
mwananchi au kiongozi bila ya kujali itikadi za ki-chama,
j. Kuondoa mwanya wa rais kujilimbikizia madaraka yanayofanana
na udikteta,
k. Kuziheshimu na kuziimarisha asasi za kiraia zisizo za serikali, na
kuzishirikisha katika uendeshaji wa nchi pale panapostahiki,
l. Kuijengea Zanzibar njia za uchumi na biashara huru na kuzilinda
kisheria rasilimali za nchi kama vile mafuta, bahari, n.k. Pia, kuipa
Zanzibar uhuru wa kutumia bandari zake na viwanja vyake vya
ndege katika kuuhuisha uchumi wake,
11.BLW lihakikishe kwamba katiba mpya ya Tanzania inajadiliwa na
kukamilika ifikapo mwezi wa Juni 2012. Endapo muda huo
hautazingatiwa, au maagizo ya BLW hayatopewa kipau mbele, au
mustakbali mwema kwa Zanzibar hautaonekena katika mchakato mzima
wa katiba mpya ya Tanzania, BLW lichukue hatua ya kuiandika upya
Page 5 of 5
katiba ya Zanzibar na kuyaingiza angalau mambo yaliyomo katika
mapendekezo haya kabla ya uchaguzi unaofuata.
MUWAZA inaihimiza serikali adhiimu ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK)
pamoja na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa kisiasa
hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba mpya ya Tanzania.
Aidha, MUWAZA inaipa hadhari SUK na BLW kukwepa mtego wowote
utakaotokea wakati mjadala wa katiba mpya utakaposhika kasi, kama vile
kutiwa katika mazonge au mgogoro utakaowagawa Wazanzibar kwa njia
yeyote ile.
MUWAZA inaziomba asasi za kiraia kuwaelimisha Wazanzibari ili waungane kwa
kauli moja katika kutetea haki za nchi yao. Elimu hiyo ni muhimu ili kutoa
nafasi nzuri kwa Zanzibar kujikita katika kulishughulikia ipasavyo suala
muhimu la katiba mpya ya Tanzania.
MUWAZA inaamini kwamba mjadala wa kuipata katiba mpya ya Tanzania ni
fursa muhimu katika kuuzaa upya na kuudumisha muungano wa aina ya
Shirikisho na kuupatia ridhaa ya washirika wake.
Hivyo basi, ni wajibu wa kila Mzanzibari mwenye kuipenda nchi yake kujidhatiti
katika kuilinda nchi yake kwa sababu pindipo Wazanzibari tutaipoteza fursa hii
adhiimu, tutakuwa hatuna wa kumlaumu wala njia ya kujinasua kwani
muungano huu tunaoulalamikia siku zote utaonekana kama kwamba
umehalalishwa na wananchi wenyewe.
MUWAZA inaamini kwamba Zanzibar inahitaji kujiimarisha ndani ya muungano
wa Tanzania sambamba na kujiimarisha kimataifa katika mamlaka na haki
zake za kitaifa. Mwanzo wa safari hiyo ni kuirudisha serikali ya Tanganyika
ndani ya muungano huo.
Kama ilivyo kawaida yake, MUWAZA itaendelea kutoa maoni yake kuhusu
mustakbali wa kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania kadri mchakato wake
utakavyoendelea.
Kwa niaba ya MUWAZA, imetolewa na:
Dr. Yussuf Saleh Salim
Mwenyekiti wa MUWAZA
Copenhagen, Danmark
Februari 5, 2011
No comments:
Post a Comment