Saturday, 5 February 2011

Msekwa akiri fedha zimeigawa CCM

<><>
 
 
Makamu mwenyekiti wa CCM,Pius Msekwa
Leon Bahati
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa ametaja utovu wa nidhamu na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali na viongozi wa CCM kuwa miongoni mwa changamoto zinazokikabili chama hicho tawala tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977.

Hata hivyo, Msekwa amesema kuwa CCM imejiandaa kujifanyia marekebisho makubwa na hata kuongeza udhibiti wa nidhamu kwa viongozi serikalini na ndani ya chama.

Msekwa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusu maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 34 tangu izaliwe Februari 5, 1977.

Kauli ya Msekwa imekuja siku moja tu tangu Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, aonye kuwepo kwa tabia ya baadhi ya viongozi kujilimbikizia mali kwa njia za ufisadi na kuwaacha wananchi wakiishi kwenye umaskini mkubwa.

Akizungumza juzi katika kumbukumbu za miaka 25 tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Samora Machel, Warioba alisema tabia hiyo ndio inayowafanya wananchi waichukie Serikali yao.

Lakini, jana Msekwa pamoja na kubainisha kasoro hizo katika uongozi ndani ya CCM na Serikali yake, alitamba kuwa, chama hicho kinajivunia mafanikio mengi ikiwamo kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar, kujenga utawala wa sheria, kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa na kujenga misingi ya soko huria.

“Kwa upande wa changamoto, nazo tumezipata. Nazo ni kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa viongozi wetu. Vingozi waliopo kwenye chama, waliopo serikalini na mojawapo ni pamoja na kusaini mikataba mibovu ambayo imeleta mateso kwa wananchi kurudisha nyuma uchumi wetu,” alisema Msekwa.

Lakini alisema katika kumomonyoka huko kwa maadili, CCM haipaswi kulaumiwa, kwa sababu iliweza kuweka vyombo vya usimamizi wa kudhibiti nidhamu isipokuwa vilishindwa kufanya kazi yake sawasawa.

Alisema kwa upande wa Serikali kuna Sekretarieti ya  Maadili ya Viongozi wa Umma, ambayo pamoja na uwepo wake alikiri kuwa haikutekeleza wajibu wake vizuri.

Msekwa ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Ukerewe, alisema kushindwa kwa tume hiyo kudhibiti nidhamu ya viongozi, kulitoa mwanya kwa baadhi ya watendaji wasio na maadili kutumia vibaya mali za umma.

Ndani ya CCM, Msekwa alisema kuna kamati za maadili katika ngazi zote za chama, lakini nazo zilishindwa kutekeleza wajibu wake.

Matokeo yake, alisema viongozi kadhaa wametumia vibaya madakara yao kwa kuendekeza vitendo vya rushwa na kuunda makundi ambayo yamekigawa chama.

Alitoa mfano vitendo vya rushwa vilivyojitokeza katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho katika kuwapata wagombea wake wa ubunge na madiwani.

Aliielezea vitendo hivyo kuwa viliwakatisha tamaa wanachama wema ndani ya CCM na hata kusababisha makundi.

Kwa mujibu wa Msekwa, makundi hayo ndiyo yaliyosababisha CCM kukosa baadhi ya majimbo na kata katika uchaguzi wa mwaka jana, ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2005.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, CCM ilipoteza majimbo 19 ya uchaguzi ambayo ilikuwa iliyapata kupitia uchaguzi wa mwaka 2005.

“Mwaka 2005 tulishinda katika majimbo ya uchaguzi 208, lakini katika uchaguzi uliopita tumepata 187. Sasa kwa kupiga mahesabu unaweza kutambua viti vingapi tulipoteza,” alisema Msekwa, ambaye aliwahi kuwa spika wa Bunge.

Kutokana na mazingira hayo, Msekwa anasema, “kwa hivyo, suala kubwa ambalo tunajitahidi kuhakikisha tunalitatua katika kipindi hiki ambacho CCM inatimiza miaka 34 ya kuzaliwa ni kupambana na kumomonyokewa kwa maadili ya viongozi wetu.”

Alisema CCM tayari imefahamu kasoro zote zilizojitokeza miaka ya 34 iliyopita na kazi iliyopo mbele yao ni kuhakikisha kwamba wanazitafutia dawa ya kudumu ili chama hicho tawala kiendelee kuaminiwa na Watanzania wengi.

Kwa upande wa mafanikio, alisema kuwa wamefanikiwa kuweka nchini utawala unaoongoza kwa misingi ya sheria na utawala bora.

Msekwa alitaja mafanikio mengine kuwa ni kubadilisha mfumo wa sera zake kutoka zile za ujamaa zinazosema uchumi utasimamiwa na dola hadi zile za soko huria.

Hii ni kutokana na miaka ya 80 watu walipata kero kubwa. “Tukasema hatuwezi kuendelea kung’ang’ania ideology huku wananchi wakiteseka, tukaingia kwenye soko huria, wananchi wakapata nafuu. Hizo zilikuwa ni sera za CCM za miaka ya 90,” alisema Msekwa.

Alisemea jambo jingine ambalo CCM inajivunia ni kusimamia mabadiliko ya mfumo wa siasa za Tanzania kutoka chama kimoja kwenda mfumo wa vyama vingi.

Kuhusu suala la Zanzibar kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Msekwa alisema hii nayo ni moja ya mafanikio ya CCM katika kipindi hicho.

“Matatizo makubwa yalitokea kabla ya uhuru na hata baada ya uhuru. Zanzibar kumetokea machafuko makubwa sana historia inaoonyesha na watu wakawa wanauawa,” alisema akifafanua:

“Lakini kutokana na umakini wa CCM, tuliweza kuwa na mazungumzo na CUF hadi tukafanikiwa kuzaa matunda ya serikali ya pamoja na tatizo limekwisha. Karibuni tulifanya uchaguzi, ulimalizika vizuri na pande zote zikakubaliana na matokeo. Hii ni mafanikio makubwa tunajivunia,” alisema.

No comments:

Post a Comment