Saturday, 5 February 2011

Makamba: Ruksa kuhama CCM kuipinga Dowans

 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, amesema ni ruksa kwa mwanachama yeyote anayetaka kuhama chama hicho kupinga malipo ya fidia kwa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited kwa sababu alijiunga nacho kwa hiari yake.
Makamba alitoa kauli hiyo jana wakati wa mahojiano na NIPASHE kufutia tishio lililotolewa na wanachama wa CCM Wilaya ya Rorya, mkoani Mara kuwa wanatarudisha kadi za chama hicho kama serikali itakubali kulipa fidia ya Sh. bilioni 94 kwa Dowans.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Rorya, Gerald Samwel, juzi alisema wanachama na viongozi mbalimbali ngazi ya kata na matawi wamekuwa wakimiminika katika makao makuu ya ofisi za CCM wilaya na kusema kuwa hawatakuwa tayari kuendelea kuwa ndani ya chama hicho ikiwa fedha hizo zitalipwa kwa Dowans.
Makamba alisema uamuzi wa mwanachama kuingia na kutoka ndani ya chama ni hiari yake, hivyo CCM haiwezi kumzuia anayetaka kukihama kutokana na sakata la Dowans.
Kuingia ndani ya chama ni hiari, kutoka chama ni hiari, kwa hiyo sisi hatuwezi kuwa na ujanja wa kumzuia mtu anayetaka kurudisha kadi kwa kuwa hiyo ni hiari yake, kwani aliingia ndani ya chama kwa hiari yake, akiamu kurudisha kadi ni hiari yake mwenyewe na katiba ndivyo inavyosema,” alisema Makamba.
Hata hivyo, Makamba alisema kauli ya Samwel inatia mashaka kwa sababu kwanza hajazungumza na wanachama wote wa CCM wa wilaya hiyo kubaini kama ni msimamo wa wanachama wote, hivyo chama kinachukulia kauli hiyo kama ni maoni yake binafsi.
Alisema hata kama yatakuwa ni mawazo ya wanachama wote wa CCM wilaya ya Rorya, uongozi wa CCM hauwezi kuwazuia kuhama kwa sababu walichukua kadi za kujinga kwa hiari yao, hivyo hata wakiamua kurudisha kadi itakuwa ni hiari yao wenyewe.
Makamba alisema kama wanachama hao watachukua uamuzi huo kimsingi, hali hiyo haitaweza kukiathiri chama kwa sababu tabia ya wanachama kuhama chama haijaanza leo wala kesho, lakini bado CCM inaendelea kuwepo.
Suala la kuhama wanachama halijaanza leo, alikuwepo Mrema (Austibe Mrema, Mwenyekiti wa TLP) alihama CCM, lakini chama bado kipo, hata viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani walikuwepo CCM wakati wa mfumo wa chama kimoja na baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza walihama CCM, lakini CCM imeendelea kuwepo hadi sasa,” alisema Makamba.
Alisema wanachama wa CCM lazima watambue kuwa chama siyo mali ya mtu bali ni mali ya watu hivyo hata kama akihama Makamba (Katibu Mkuu) kitaendelea kuwepo kwani chama cha watu hakifi akitoka mtu kwasababu CCM siyo mali ya mtu.
Tangu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) wa kuiamuru Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kuilipa kampuni ya Dowans Tanzania Limited kumekuwa na matamko mbalimbali yanayokinzana juu ya fikia hiyo.
Maamuzi ya fidia hiyo imepokewa kwa hisia hasi na wananchi wengi, wakiitaka serikali kukataa kuilipa pamoja na kuwashughulikia waliongia mkataba huo katiya Tanesco na Dowans. Dowans ilirithi mkataba tata wa Richmond ambao iliingia na Tanesco Juni 23, 2006 kwa ajili ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100. Richmond ilishindwa kazi hiyo, iligundulika kuwa kampuni ya mfukoni, isiyo namtaji na ilidanganya wakati wa mchakato wa kufikiwa kwa mkataba huo.
Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato huo iligundua kuwako kwa udanganyifu na kuingilia kwa baadhi ya viongozi katika kufanikisha Richmond kupata kazi hiyo wakati haikuwa na uwezo si kifedha wala kitaalam kutekeleza maradi huo. Ripoti ya kamati hiyo ndiyo ilisababisha Februari 2008 kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na mtangulizi wake kwenye wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha (Ushirikiano Afrika Mashariki).

MBATIA APINGA MALIPO
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameitaka Serikali kutolipa fidia ya Sh. bilioni 94 kwa Dowans, badala yake iwafilisi waliongia mkataba mbovu wa Richmond uliorithiwa na kampuni hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alisema hakuna sababu yoyote ya kuilipa Dowans wakati walioingia katika mkataba mbovu iliyourithi wapo.
Tunatambua kuwa wapo watumishi wa Serikali pamoja na baadhi ya wanasiasa ambao walihusika kuingia mikataba mbovu na Dowans, kwa nini wachukue mali ya Watanzania ndio walipe deni hilo?” alihoji.
Aliongeza: “Tunamuomba Rais awakamate watumishi na wanasiasa waliohusika katika kuingia mikataba hiyo, atathmini mali zao zote zifilisiwe ndio walipe hilo deni la Sh. bilioni 94, na kama mali zao hazitatosheleza basi wapelekwe jela, kinyume cha hapo inaweza kuondoa kabisa usalama wa nchi yetu, kama tunavyoona nchi za wenzetu kwa sababu wananchi wengi wanaumia sana.”
Alisema itasikitisha sana kama Serikali itawalipia mafisadi deni wakati wanafuzi wa vyuo vikuu wakiendelea kuhangaishwa na mikopo huku baadhi ya wafanyakazi wanaotumikia wananchi wakiwa wanasota kudai malipo yao, na kutolea mfano wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa nini tukaribishe Tunisia nchini kwetu kwa ajili ya mafisadi, kupoteza fedha kwa ajili yao wakati wanafunzi wetu wanahangaishwa kupewa mikopo, eti Dowans ndio tunataka kuwalipa harakaharaka,” alisema na kuongeza:
Ina maana za harakaharaka za kulipa Dowans zipo ila za wanafunzi au wazee wa Afrika Mashariki hazipo. Hili kweli ni jambo la kusikitisha.”
Aliwapongeza wanaharakati ambao wamepeleka pingamizi mahakamani kupinga uamuzi wa serikali wa kutaka kuilipa Dowans.
Tunawapongeza sana baadhi ya viongozi wetu ambao wamepeleka pingamizi mahakamani, wameonyesha kwa dhati kuwa jambo hili linawauma, pia jinsi gani wanajali maslahi ya Watanzania,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment