Sunday, 6 February 2011

BoT yatetea noti za 'batiki'

*Ni zile mpya zilizotolewa hivi karibuni
*Yadai zimetengenezwa kwa teknolojia mpya
*Yadai zikisuguliwa na kuacha rangi ndio halali 


Na Rehema Mohamed

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa ufafanuzi kuhusu kuchuja rangi  katika
noti mpya zilizotolewa hivi karibuni na kusema kuwa hali hiyo ni ya kawaida kwa noti zilizochapwa kwa teknolojia maaluum ijukanayo kama 'Intaglio Printing'

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alisema aina hiyo ya uchapishaji unafanya noti kuwa na hali ya mparuzo zinapopapaswa na imetumika ili kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kuchanika na kuchakaa kwa haraka.

Prof. Ndulu alisema miparuzo hiyo huacha rangi noti inaposuguliwa kwa nguvu kwenye karatasi nyeupe kitendo ambacho kinathibitisha kuwa noti hiyo ni halali.

"Kutoa rangi ni moja ya alama ya usalama inayothibitisha kuwa noti siyo bandia, noti hizi hazichuji zikilowekwa kwenye maji kama inavyodaiwa kwa kuwa wino uliotumika hauyeyuki kwenye maji,"alisema Prof.Ndulu

Prof.Ndulu alisema kuwa utowaji rangi huo upo hata katika noti za nje kama dola pale zinaposuguliwa ambapo teknolojia iliyotumika kutengezewewa inalingana.

Alisema kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ya kuwekewa kinga dhidi ya uchafu ili kupunguza uwezekano kunasa uchafu inapokuwa katika mzunguko.

Aliongeza kuwa noti za zamani bado ni halali na zitaendelea kutumika pamoja na zile mpya mpaka zitakapopotea katika mzunguko kwa sababu ya uchakavu wake.

Akizungumzia hoja ya kuwepo noti mmoja iliyo na thamani kubwa zaidi ya ile ya sasa ya sh.10,000/-, Prof. Ndulu  alisema BoT haikuona haja ya kufanya hivyo kwakuwa malipo makubwa yanahimizwa kufanywa kupitia njia nyingine za kibenki kama njia ya mitandao.

Katika siku za karibuni wananchi mbalimbali wamekuwa wakilalamika na kuhofia teknolojia iliyotumika kutengeza noti mpya zilizotolewa hivi karibuni.

Noti hizo ambazo ni ya 10,000/-, 5,000/-, 2000/-, na  1,000/- zilipokelewa kwa shingo upande baada ya kuingizwa kwenye mzunguko na BoT huku wengine wakidai zimetengenezwa kwa teknolojia dhaifu na kulinganisha na upikaji vitenge aina ya batiki.

Hali hiyo imesababisha watu wengi kutokuwa na imani nazo huku yakiwepo matukio ya msuguano katika maeneo mbalimbali ya biashara ka baadhi ya watu kuzikataa pale wanaporudishiwa chenji hususani muda wa usiku.

Hata wale wanaozipokea saa za mchana wamekuwa na mashaka nazo na kuziangalia mara mbili mbili huku wengine wakilalamika kwamba zimetengenezwakwa teknolojia ya chini inayopunguza hadhi ya noti hizo. 

No comments:

Post a Comment