Saturday, 5 February 2011

Baa Moja ya Mji Mkongwe Yaripuliwa kwa Moto



Na Salma Said Zbar
SIKU chache baada ya wananchi wa Mji Mkongwe kutoa malalamiko yao kudharauliwa amri ya mahakama ya kutaka baadhi ya baa zilizopo katika makaazi ya watu zifungwe, watu wasiojulikana wameripua na kuiteketeza kwa moto baa moja iliyopo Mji Mkongwe Zanzibar.
Wimbo hilo la watu kujichukulia sheria mikononi limeanza wiki iliyopita katika maeneo ya Darajabovu na Mwanyanya kuzichoma baa mbili zilizopo katika maeneo ya makaazi ya watu baada ya malalamiko yao ya muda mrefu kutochukuliwa hatua yoyote.
Juzi watu wasiojulikana waliiongia katika baa ya Migombani iliopo kati kati ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na kuteketeza kila kitu ikiwemo masanduku ya kuhifadhia ulevi na vitu vyengine muhimu vilivyopo katika baa hiyo.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo lililotokea majira ya saa nane za usiku, walisema kwamba moto huo ulianza baada ya kusikika mlio mkubwa wa mripuko ambapo majirani walitoka kwenda kuona kinachoendelea na kukuta moto ukiwaka eneo hilo la baa.
Kwa mujibu wa mlinzi aliyekuwepo katika lindo la baa hiyo alisema awali aliwaona watu wawili wakiingia ndani ya jengo hilo na baada ya muda mdogo akasikia mlio wa risasi ambapo walipigwa mbwa wawili waliokuwepo katika baa hiyo kwa ajili ya ulinzi ambapo mbwa mmoja aliuliwa baada ya kupigwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi baada ya kubweka kwa sauti kubwa.
“Nimesikia kishindo kikubwa cha mlio kama vile kitu cha kuripuka na sio muda mrefu nikamuona mbwa wetu mmoja amelala na kufariki dunia hapo hapo nadhani ilikuwa ni risasi lakini sina hakika hiyo….alisema mlinzi huyo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Mohammed alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi zaidi unaendelea ili kujuwa chanzo cha tukio kwani hivi sasa kumeibuka vitendo hivyo kwa kasi.
“Tumepata taarifa ya tukio hilo la kuchomwa moto kwa baa mmoja iliopo katikati ya Mji Mkongwe…hatujajuwa chanzo chake kinatokana na nini lakini tutatoa taarifa baada ya kufuatilia kwa kina chanzo na sababu za moto huyo kwa sababu hatuwezi kutoa taarifa wakati watu wetu ndio wanafanya hiyo kazi ya kiuchunguzi” alisema Kamanda huyo.
Mkurugenzi wa baa hiyo na mmiliki wa biashara hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Christopher John Makata alisikitishwa na kitendo hicho cha kuripuliwa baa yake ambapo amesema amepata hasara kubwa kutokana na mali yake iliyokuwa ikihifadhiwa ndani ya baa hiyo kuteketea kwa bila ya kubaki kitu.
Makata alisema kwamba wakati moto huo unateketeza baa hiyo kulikuwa na jumla ya kreti mia sita (600) za bia pamoja na vinywaji vyengine vikiwemo soda na maji ya chupa ya aina mbali mbali ambazo zilikuwa zikiuzwa katika baa hiyo.
Aidha alikiri kupata hasara kubwa inayofikia zaidi ya shilingi milioni 60 na kusema kwa sasa anafikiria kuhamisha biashara zake Zanzibar kufuatia kupata mkasa huo ambao umerudisha nyuma maendeleo ya maisha yake.
“Nimepata hasara kubwa ya kuchomwa moto kwa baa yangu maisha yangu nategemea biashara zangu ikiwemo hii baa, mali zangu zote zilizokuwa zimehifadhiwa katika chumba cha akiba kwa hivyo kuteketea kwa moto katika baa yangu kumemaliza kila kitu changu”alisema Makata.
Uchunguzi zaidi unaonesha kwamba baa ya Migombani ambayo ipo kati kati ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ilikuwa na mgogoro wa muda mrefu na wakaazi wa eneo hilo ambao waliweka pingamizi mahakamani kupinga uhalali wa kufanya biashara eneo hilo.
Khaleed Said Gwiji anasema suala la baa katika Mji Mkongwe linawakera wakaazi wengi kwa kuwa baa hizo mbali ya kuwa katika maeneo ya makaazi ya watu lakini baadhi yao zipo karibu na nyumba za ibada na kibaya zaidi ni kuwa zinaendesha biashara za ukahaba na kupiga miziki usiku kucha jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wakaazi wa eneo hilo.
Hata hivyo baa hiyo ambayo tokea mwaka jana kesi yake ambayo ipo katika ngazi ya kukatiwa rufaa ingawa kesi hiyi imekuwa ukisuasua jambo ambalo wakaazi wa Mji Mkongwe wakilalamika kwamba haikupaswa kisheria kuendesha biashara zake hadi hapo uamuzi wa mahakama utakapotolewa lakini ilikuwa ikiendelea na biashara zake kama kawaida.
“Huu ni mwaka mmoja sasa wananchi tunasubiri kusikilizwa kwa rufaa ya pingamizi la mfanyabiashara huyo bila ya mafanikio wakati biashara ya ulevi katika eneo hilo ikiendelea kitendo chake cha kuuza bia kama kawaida nadhani ndicho kilichowatia watu hasira hizo” alisema mkaazi mmoja wa Mji Mkongwe ambaye anaishi karibu na baa hiyo.
Alisema wakaazi wa Mji Mkongwe wamekuwa na kilio cha muda mrefu kutoka na kuenea kwa baa katika mkaazi ya watu jambo ambalo biashara za uhahaba, wizi na upigaji wa miziki kwa sauti kubwa ni miongoni mwa malalamiko ya wakaazi hayo jambo ambalo serikali haijalichukuliwa hatua za kakusudi kukabiliana na kero hizo za wananchi.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi wananchi wameilalamikia baa ya Dharma Lounge, iliuopo Vuga, wananchi wa Mji Mkongwe wamesema kuwepo kwa baa hiyo kunachochea vitendo vya uhalifu katika eneo hilo ikiwemo kufanyika vitendo vya kuuza miili na kufanya fujo za miziki usiku kucha.
Wananchi hao walisema Dharma Lounge ni miongoni mwa baa zinazoendelea kuchangia kero hiyo licha ya Mahakama ya Vileo ya Mwanakwerekwe kutoa amri ya kufunga baa hiyo lakini bado inaendelea na shughuli zake kama kawaida.
Amir Hamza Amir, Khaleed Said Gwiji, na Raya Ali ambao ni wote ni wakaazi wa Vuga eneo la Mji Mkongwe wamesema serikali inapaswa kusimamia vyombo vyake kwa kuhakikisha sheria zinafuatwa.
Amir alisema kuendelea kuwepo kwa shughuli za baa hizo katika eneo lao kunachochea kasi ya mmomonyoko wa utamaduni, mila na desturi za Zanzibar zinazozingatia misingi ya dini jambo ambalo serikali inatakiwa kuingilia kati suala hilo .
Kwa mujibu wa hati iliyotolewa na Mahakama ya Vileo ya Mwanakwerekwe Januari 24, mwaka huu, baa ya Dharma Lounge pia imenyimwa leseni kwa kipindi cha mwaka 2011.
Uamuzi huo, kwa mujibu wa hati hiyo ambayo gazeti hili pia imepata nakala yake ilitolewa na Hakimu Abdulrazak Ali ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Mahakama ya Vileo ya Mwanakwerekwe.
Hakimu Ali akitoa uamuzi huo, alikataa ombi la Dharma Lounge kuongezewa muda kw akupew akibali cha mwaka huu wa 2011 na kusema kwamba baa hiyo haitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake katika eneo hilo kutokana na wananchi wa eneo hilo kukataa baa hiyo katika eneo lao.
“Ombi limekataliwa. Muombaji asipewe leseni ya 2011, kwa sababu majirani zake hawataki baa yake,” alisema Ali katika hati hiyo ya mahakama ya Manakwerekwe iliyotolewa uamuzi januari 24 mwaka huu.
Wiki iliyopita baa ya Peace Love iliopo Daraja bovu pamoja na baa iliopo Mwanyanya zilichomwa moto kwa madai kwamba zinaendesha biashara ya ulevi katika maeneo wanayoishi wananchi.
Hadi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijasema lolote kuhusiana na suala hilo la kuripuliwa kwa moto baa ambapo kwa mujibu wa sheria wamiliki wa baa hizo hukata leseni katika mamlaka zinazohusika za biashara hiyo.
Biashara ya ulevi inaendeshwa katika maeneo mengi ya Unguja na Pemba ambapo hivi sasa kumekuwepo na utitiri wa vilavu vya pombe katika maeneo ya wazi, makaazi ya watu pamoja na karibu na sehemu za nyumba za ibada jambo ambalo kwa mujibu wa sheria hairuhusiwi kufungua baa katika maeneo kama hayo lakini baa hizo zimekuwa zikiendeshwa bila ya kufuata sheria za vileo.
Karibu asilimia 25% ya mapato yanayokusanywa na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) yanatokana na vinywaji vikali vya vileo pamoja na soda katika mahoteli ya kitalii Zanzibar na baa za mitaani.
Kama matukio ya uchomaji moto na uharibifu wa hoteli za kitalii utaendelea basi unaweza kabisa kuharibu mapato ya nchi ambayo yanategemea sekta ya Utalii ikiwemo vinywaji vya vileo.

No comments:

Post a Comment