Sunday, 23 January 2011

Utata waibuka ukodishwaji wa majengo na fukwe Z`bar





Mpango wa kukodisha majengo mawili ya historia na ufukwe wa Shangani ulikiuka taratibu kwa kufanyika bila kupitishwa na Baraza la Mawaziri Zanzibar, imethibitika.
Majengo hayo, maarufu 'Mambo Msige' yamekodishwa kwa Kampuni ya Kempiski Group Hotel kwa dola za milioni 1.5 sawa na shilingi bilioni mbili kwa muda wa miaka 99 kuanzia Oktoba mwaka jana.
Ukodishaji huo ulifanywa na Serikali ya awamu ya sita na kusababisha taasisi zilizokuwa zinatumia majengo hayo zimeanza kuhamia sehemu nyingine.
Uchunguzi wa Nipashe Jumapili, umebaini kuwa hakuna kikao cha Baraza la Mawaziri kilichokaa kujadili na kupitisha mpango wa ukodishaji huo.
“Baraza la Mapinduzi hatujawahi kujadili na kupitisha mradi huo, hili ni jambo geni kwangu inawezekana lilijadiliwa na kupitishwa nje ya baraza la Mawaziri,” alisema waziri mmoja wa mawaziri wa serikali ya awamu ya sita huku akiomba kuhifadhiwa jina lake.
Hata hivyo, alisema iwapo suala hilo lingewasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri yeye angekuwa wa kwanza kupinga kwa vile thamani ya majengo na ufukwe uliokodishwa hailingani na thamani ya fedha iliyolipwa chini ya makubaliano anayosema yalifanyika ‘kinyemela.’
Alisema chini ya misingi ya uwazi, kabla ya ukodishaji huo serikali ilipaswa kutangaza zabuni ili kutoa nafasi ya kushiriki waombaji wengi, wakiwemo wazawa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Jaji Omar Othman Makungu, alisema kwa upande wake hawezi kuzungumzia mkataba huo kwa vile hakuwemo katika safu ya uongozi wa juu wa serikali ya awamu ya sita.
“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na mkataba huo, nimeteuliwa hivi karibuni na kukuta jambo hilo limekwishafanyika, lakini naamini taratibu zilifuatwa,”alisema Jaji Makungu.
Lakini mjumbe mmoja wa Baraza la Wawakilishi, alisema meamua kupeleka barazani hoja ya kupinga ukodishwaji wa majengo hayo na ufukwe kwa maelezo ulifanyika bila kuzingatia maslahi ya taifa.
“Zabuni haikutangazwa na thamani ya mali haiwiani na fedha zilizolipwa…muda wa ukodishaji pia ni mrefu,” alisema mwakilishi huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Alitoa mfano wa jengo la Wizara ya Elimu ambalo alisema limekodishwa kwa thamani ya dola milini 2.5 tofauti na dola 1.5 zilizolipwa na Kampuni ya Kempski Group Hotel kwa kukodisha majengo mawili na viwanja vitatu kwa miaka 99.
Mmiliki mpya wa eneo lililokodishwa anakusudia kujenga hoteli ya nyota tano yenye ghorofa tano kinyume na masharti ya uhifadhi wa Mji Mkongwe ambao umeweka ghorofa tatu kuwa mwisho kwa majengo katika mji huo.
Tayari masharti hayo yamesababisha mmiliki mpya wa eneo hilo kutoendelea na kazi za awali za ujenzi baada ya Mamlaka ya Mji Mkongwe kukataa kupitisha ramani mbili za ujenzi. “Hatutoi kibali cha ujenzi hadi hapo masharti ya uhifadhi mji Mkongwe yatakapozingatiwa, ndio maana michoro miwili ya ramani za ujenzi zimeshindwa kupitishwa katika mradi huo,” alisema Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Issa Makarani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi, inayoshughulikia masuala ya ujenzi na ardhi, Makame Mshimba, alisema kamati yake itafuatilia kujua mazingira yanayozidi kuibuka juu ya mradi huo.

No comments:

Post a Comment