Sunday, 23 January 2011

Mbunge aliyeshindwa’ atekeleza ahadi




na Janet Josiah, Tandahimba
ALIYEKUWA mgombea ubunge wa jimbo la Tandahimba kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Katani Ahmed Katani, ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa kwa wananchi kwa kuwaletea mradi wa maji na kujenga kituo cha afya cha kijiji hicho.
Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wananchi wa Luagala, Katani alisema ingawa alinyang’anywa nafasi yake ya ubunge na kufuatilia haki yake mahakamani, ameweza kutekeleza ahadi ya kuwapa wananchi wa Luagala mifuko 200 ya simenti kwa ajili ya kujenga kituo cha afya.
Mbali na kuanza kujenga kituo cha afya, Katani aliwaeleza wananchi hao kuwa tayari amekwishazungumza na wafadhili wa mradi wa maji kutoka Ujerumani ambao wataanza kuwasambazia huduma hiyo Aprili mwaka huu.
Sambamba na miradi hiyo, Katani alisema anaendelea kujipanga kujenga shule za msingi katika vijiji ambavyo bado vinapungukiwa shule na kuwalazimu watoto wa vijiji hivyo kutembea zaidi ya kilometa 12.
“Huku nikiendelea kusubiri haki yangu toka mahakamani na si siku nyingi ni miezi sita tu ijayo …. Naendelea kutekeleza ahadi zangu kwani uwezo wa kufanya hivyo ninao,” alisema Katani.
Wakati wa kampeni za uchauzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, mgombea huyo aliwaahidi wananchi hao kuwatatulia tatizo la maji, kujenga shule za msingi, kituo cha afya cha Luagala, tarafa ya Kitama pamoja na kushughulikia uuzaji na zao kuu la korosho.
Hata hivyo katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Juma Njwao alitangazwa kuwa mshindi.

No comments:

Post a Comment