Sunday, 23 January 2011

Mawaziri, wabunge wa CCM wafundwa


  Wapigwa marufuku kutoroka bungeni
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewafunda mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa wa kweli na kujibu hoja zinazowahusu kwa wakati unaofaa ili kujenga imani kati ya serikali na wananchi.
Kadhalika, alisema kuanzia bunge lijalo ni marufuku kwa mawaziri kutoroka vikao vya bunge bila sababu za msingi kama ilivyokuwa vikao vilivyopita.
Waziri Pinda, alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua semina ya siku tatu kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa chama hicho.
Aidha, alisema semina hiyo iwe fursa ya kumaliza chuki zilizopo miongoni mwao ili kuongeza mshikamano kwa kuwa wanapovurugana inakuwa ni mwanzo wa kuwachanganya Watanzania wote.
"Kwanza kabisa nawaasa Mawaziri kuwa wakweli, wajibu hoja kwa wakati ili kuboresha utendaji wetu... mmepata fursa ya kukutana katika semina hii, chuki katika chama zimalizike kuanzia sasa mshikamane," alisisitiza.
Aliongeza kuwa wabunge kupitia chama hicho ni lazima wajiendeleze kielimu ili wanapotoa hoja ziwe nzito kutokana na Bunge la sasa kuwa na idadi kubwa ya wapinzani.
"CCM ina wabunge 260 na kwamba asilimia 60 ya wabunge hao ni wapya kabisa, hivyo ni vyema wakajifunza na kujua kanuni za bunge na wajibu wake kupitia semina hiyo," alisema Waziri Mkuu Pinda.
Alisema mbunge wa CCM anatakiwa kuwa jasiri awapo bungeni sambamba na jimboni mwake ikiwemo kusikiliza kero na hoja zinazotolewa na wapiga kura wake.
Semina hiyo iliyofunguliwa jana na Waziri Mkuu Pinda itaendelea leo na kesho ambapo Rais, Dk. Jakaya Kikwete anatarajia kuifunga.

No comments:

Post a Comment